June 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yanywea kwa Lissu, MAWIO

Spread the love

MPANGO wa upande wa Jamhuri, kurudisha mashitaka yaliyofutwa katika kesi cha uchochezi inayomkabili Tundu Lissu, Jabir Idrissa, Simon Mkina na Ismail Mahboob umeshindikana, anandika Faki Sosi.

Lissu ni Mbunge wa Singida Mashariki; Jabir ni Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la MAWIO, Mkina ni Mhariri Mkuu wa gazeti hilo na Mahboob ni Meneja wa kampuni ya uchapishaji wa magazeti ya Flint.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, upende wa mashtaka ulipanga kusoma upya mashitaka ambayo waliyafuta wenyewe mahakamani hapo baada ya kukubaliana na hoja za utetezi kuwa, mashtaka hayo hayana miguu ya kusimama kisheria.

Upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili Kishenyi Mutalemwa pamoja na Nassoro Katuga wamefika mahakamani hapo wakiwa na hati yenye mashitaka mapya kwa madai kuwa, mshitakiwa namba moja Jabir Idrissa amefika mahakamani hapo kwa mara ya kwanza.

Upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Peter Kibatala, umepinga kurudishwa kwa mashtaka hayo kwa madai kuwa, mashitaka hayo yalifutwa kutokana na Upungufu wa kisheria ambapo Jamhuri wangeweza kuyarudisha mashitaka hayo baada ya kufutwa kwa misingi ya kifungu cha 255 au wakate rufaa.

Kibatala ameeleza zaidi kuwa, serikali ndiyo ilikubali kuondoa mashtaka hayo na kukiri mbele ya mahakama kuwa, mashtaka hayo hayana mashiko.

Wakili Mutalemwa, aliomba muda wa saa moja, kupitia makabrasha ya kisheria ili aweze kujibu hoja za utetezi, ambapo hakimu alitoa muda wa saa moja.

Baada ya muda ule kufika, Lissu alichelewa kufika kizimbani hapo, jambo lililozusha mjadala mwingine kwa upande wa Jamhuri kuitaka mahakama imchukulie hatua.

Mjadala huo ulikoma mara baada ya kuonekana Lissu akiingia kortini, ambapo upande wa serikali ulianza kujibu hoja zilizotolewa na utetezi.

Kishenyi amedai kuwa mshitakiwa wa kwanza, anatakiwa kusomewa tena mashtaka yake ili ajibu, ambapo anatakiwa asomewe mashitaka matano na wasomewe kwa pamoja.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Thomas Simba, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, ameamaru upande wa Jamhuri usome mashitaka kwa mshitakiwa namba moja (Jabir) na washitakiwa wengine ili wajibu mashtaka hayo.

Hakimu Simba amesema, uamuzi wa hoja zilizobishaniwa utatolewa tarehe 15 Septemba, 2016 juu ya kurudishwa kwa mashitaka yaliyofutwa.

Wakili Kishenyi, akisoma mashtaka matatu yaliyobaki kwa washitakiwa, amedai kuwa shitaka namba mbili linamkabili mtuhumiwa namba moja, mbili na nne (Jabir, Mkina pamoja na Lissu), kwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika Gazeti la MAWIO, toleo namba 182 la tarehe 14-20 Januari, 2016 lenye kichwa cha habari, ‘Machafuko yaja Z’bar’.

Shitaka namba tatu, linamkabili Ismail Mahboob, mshitakiwa namba tatu, anayetuhumiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika Gazeti hilo la MAWIO toleo namba 182 la tarehe 14-20 Januari, 2016 lenye kichwa cha Habari ‘Machafuko yaja Z’bar’.

Shitaka la nne linalomkabili mshitakiwa namba tatu pekee pia, akishitakiwa kwa kuchapisha gazeti bila kupeleka kiapo kwa msajili wa magazeti ambapo alichapisha gazeti Gazeti la MAWIO toleo namba 182 la tarehe 14-20 Januari 2016 lenye kichwa cha Habari ‘Machafuko yaja Z’bar’.

Watuhumiwa wote walikana mashtaka hayo ambapo kesi hiyo itatajwa tena tarehe 8 Septemba mwaka huu, kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

error: Content is protected !!