January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yamzuia Lowassa Taifa

Spread the love

SERIKALI imezuia matumizi ya Uwanja wa Taifa (Uhuru) wa Temeke, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli za kisiasa. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea)

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene amesema leo ofisini kwake kwamba marufuku hiyo imekuja baada ya kuwepo taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepanga kufanya mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake kwenye uwanja huo.

“Serikali haitaruhusu chama chochote cha siasa kuutumia uwanja wa taifa kwa shughuli za kisiasa ili kuepuka matukio yanayoweza kutokea kwa mihemko ya kisiasa,” amesema Mwambene ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.

Amesema Chadema ilipeleka barua serikalini kuomba kutumia uwanja huo kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni utakaofanyika Jumamosi ya Agosti 22; hata hivyo majibu ni kuzuiwa kwa matumizi ya uwanja huo kwa shughuli za kisiasa zikiwemo hizo za kampeni.

Haikuweza kuthibitishwa kama ni kweli Chadema iliandika barua serikalini kuomba kutumia uwanja huo, lakini hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikusudia kufanya mkutano wake wa uzinduzi wa kampeni kwenye uwanja huo.

Chama hicho kimemteua Edward Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu Februari 2008 kwa kutuhumiwa kuingilia zabuni ya kufua umeme iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC), kuwa mgombea urais wa Tanzania.

Siku mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli alipotoka kuchukua fomu za uteuzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rais Jakaya Kikwete aliyempokea kwenye uwanja wa Ofisi Ndogo za CCM Lumumba, alisema uzinduzi wa kampeni ungeweza kufanyika Uwanja wa Taifa, kwa kuwa viwanja vya Jangwani vinatumika kwa shughuli za Wamachinga.

Tayari chama hicho kimetangaza rasmi kuwa kitazindua kampeni kwenye viwanja hivyo vya Jangwani.

Kutokana na uamuzi wa serikali kuzuia uwanja wa taifa, Chadema kinachogombea chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) pamoja na vyama vingine vitatu, huenda kikazindua kampeni uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe, Dar es Salaam.

error: Content is protected !!