January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yamzuia Lowassa Jangwani, UKAWA wakomaa

Spread the love

MKURUGENZI wa Manispaa ya Ilala, Claud Mpelembwa amezuia mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za Urais, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa kufanyika katika viwanja vya Jangwani kwa madai ya uwanja huo kuwa na matumizi mengine. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Pamoja na kuwepo kwa barua hiyo kutoka kwa mkurugenzi wa Ilala, Umoja wa wadai Katiba ya Wananchi (UKAWA) umesisitiza kuwa ratiba ya mkutano wao utakuwa kama walivyopanga, eneo, muda na tarehe ile ile.

Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, James Mbatia aliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali imekataa ombi lao la kufanyia mkutano kwenye viwanja vya Jangwani bila ya kuwa na sababu za msingi.

Mbatia amesema waliandika barua ya 22 Agosti, 2015 kutumia viwanja vya Jangwani lakini mkurugenzi amewazuia kutumia viwanja hivyo kwa madai kuwa tayari umeshalipiwa na mtu mwingine, ambaye hakutaka kumtaka kwa sababu zao binafsi.

“Tumefanya juhudi zote za kiungwana ili tuweze kupewa viwanja hivyo ikiwemo kuomba kumjua aliyelipia ili tufanye naye mazungumzo lakini serikali ilikataa kutupa jina la mtu huyo. Tutafanya mkutano Jangwani,” amesema Mbatia.

Mwenyekiti huyo amesema hii ni mizengwe inayoanzishwa na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kujaribu kuzuia mafuriko ya mgombea wa UKAWA, lakini hilo haliwezekani kwa kuwa kwenye nguvu ya umma hakuna kinachoweza kuzuilika.

“Hivi ni vitendo vya kishetani vinavyofanywa na serikali na vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa wananchi. Tunahitaji utulivu ili tujenge Tanzania yetu, hatupo tayari kuona damu inamwagika kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine,” amesema Mbatia.

Pia Mbatia amemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Damian Lubuva afanye kazi kwa kusimamia misingi ya haki bila ya kupendelea chama chochote cha siasa.

Mbatia amesema katika uzinduzi wa kampeni za CCM wiki iliyopita, kiongozi mwandamizi wa serikali alitoa kauli za matusi na kejeli, mkutano huo ulivunja kanuni za uchaguzi kwa kupitiliza muda uliopangwa, lakini Lubuva hakusema chochote mpaka sasa.

“CCM chini ya Rais Kikwete (Jakaya) ndiyo walikuwa wa kwanza kuvunja sheria kwa kupitiliza muda wa kampeni, lakini pia walitoa maneno ya kejeli na matusi, lakini cha ajabu si serikali wala Tume iliyokemea matukio hayo,” amesema Mbatia.

Kwa upande mwingine Mbatia amelitaka jeshi la polisi kuacha kutumiwa na CCM, kwa kuwazuia baadhi ya wagombea wa chama fulani huku chama kingine kikiachiwa kufanya kile ambacho wengine wamekatazwa.

Mbatia amesema kitendo cha Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kupiga marufuku ziara za Lowassa kutembelea kwenye masoko, hospitali na sehemu nyingine, huku wagombea wa CCM wakifanya ziara hizo kwa kusindikizwa na jeshi hilo.

“Leo Lowassa (Edward) alikuwa atembee kwenye hospitali jijini Dar es Salaam, lakini Kova amezuia, huku Mgombea Mwenza wa CCM, Samia Suluhu akisindikizwa na polisi kutembelea hospitali za Rombo, Kilimanjaro. Hii siyo haki,” amesema Mbatia.

Mbatia amewatoa hofu watanzania, kuwa hawatafanya kampeni za uvunjifu wa amani bali wao watahubiri amani, na siyo kama CCM wanavyohubiri vita na kuwatisha wananchi juu ya uvunjifu wa amani.

error: Content is protected !!