August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yamwaga mikopo kwa vijana

Antony Mavunde, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini

Spread the love

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa taarifa juu ya utekelezaji wa utolewaji wa mikopo kwa vijana, anaandika Mwandishi Wetu.

Taarifa kamili ya serikali iliyotolewa na Idara ya Habari – MAELEZO hii hapa;

Dodoma, Jumatatu, tarehe 6 Februari, 2017

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo suala la Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, kubadilika kwa hali ya tabianchi na kuchelewa upelelezi wa makosa mbalimbali ya jinai. Ufafanuzi huo umetolewa mjini hapa leo.

Mikopo kwa Vijana

Serikali imesema jumla ya vikundi vya vijana 309 kutoka Halmashauri mbalimbali nchini vimefaidika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kupata mikopo yenye jumla ya shilingi 1,867,896,520. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde ameeleza.

Katika ufafanuzi wake, Naibu Waziri Mavunde ameongeza kuwa, Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) za vijana kutoka katika Halmashauri 94 pia vimefaidika na mikopo hiyo.

Ameongeza kuwa, mikopo hiyo imekuwa msingi mzuri wa maendeleo kwa vijana kwa kuwa wengi wamepata mitaji ya kuanzisha miradi kama ya kilimo, ufugaji, usindikaji wa mazao na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo.

Mazingira na Tabianchi

Akijibu hoja kuhusu suala la mazingira na tabianchi, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina amesema Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (2012) ambao umesaidia utekelezaji wa hatua mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo.

Amefafanua kuwa, baadhi ya hatua ambazo Wizara za kisekta zimekuwa

zikitekeleza ni pamoja na kuhimiza kilimo kinachozingatia mabadiliko ya misimu ya mvua, ufugaji endelevu, kuhifadhi vyanzo vya maji na misitu, ujenzi wa mabwawa ya maji, upandaji miti, matumizi ya nishati mbadala, ujenzi wa miundombinu imara ya barabara, madaraja na mifereji ili kuhimili mafuriko na matumizi ya teknolojia rafiki za mazingira viwandani.

Upelelezi wa makosa mbalimbali

Serikali imesema imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za haraka ili kukabiliana na ucheleweshaji wa kesi Mahakamani. Amezitaja hatua hizo kuwa ni kufanya ukaguzi wa majalada ya kesi unaofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kuundwa kwa Jukwaa la Haki Jinai na kutembelea mahabusu magerezani na kufanya mahojiano na mahabusu au wafungwa wenye rufaa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alipokuwa akijibu hoja kuhusu suala la kuchelewa kwa upelelezi wa makosa mbalimbali, ambapo alisisitiza kuwa pia upo muda wa kisheria wa siku 60 wa kuondoa shauri Mahakamani kama upelelezi haujakamilika.

Ushuru bidhaa za vinyago

Serikali imefafanua kuwa, vinyago sio miongoni mwa bidhaa zinazotozwa kodi au ushuru wa bidhaa zinaposafirishwa nje ya nchi (export duty). Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa, iwapo vinyago vitazuiliwa uwanja wa ndege au mpakani, sio kwa sababu ya kutolipwa kodi au ushuru wa forodha.

Ameongeza kuwa, utaratibu unaotumika kimataifa ikiwemo Tanzania katika kushughulikia bidhaa zozote zinazokamatwa kwenye sehemu za kuingia au kutokea nje ya nchi ni wa aina mbili; kuziharibu/kuziteketeza bidhaa hizo au kuzipiga mnada. Bidhaa zinazoharibiwa au kuteketezwa ni zile ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi au kwa afya ya binadamu.

Imetolewa na:

Idara ya Habari – MAELEZO.

error: Content is protected !!