January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yamtakasa Maswi sakata la Escrow

Eliakim Maswi, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Mji wa Babati

Spread the love

BALOZI Ombeni Sefue- Katibu Mkuu Kiongozi, amesema uchunguzi uliofanywa dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, haukumkuta na hatia yoyote katika kashfa ya ukwapuaji fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)… Anaadika Mwandishi Wetu (endelea).

Balozi Sefue alimsimamisha kazi Maswi kwa muda kuanzia Desemba 23, 2014, kwa kutumia madaraka aliyonayo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo makatibu wakuu ili kupisha uchunguzi dhidi yake.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari leo Ikulu jiji Dar es Salaam, Balozi Sefue, amesema uchunguzi umekamilika na Maswi amebainika kutotenda kosa lolote ya kinidhamu katika sakata hilo.

Amesema kuwa kutokana na uchunguzi huo, mamlaka ya uteuzi wake (Rais) ambayo ilikuwa imemsimamisha, imeachiwa kuamua hatua za kuchukua dhidi yake ikiwa ni pamoja na kumresha kazini au kumpangia majukumu mengine.

Wakati wa kusimamishwa kwake, Balozi Sefue alisema kuwa amechukua hatua hiyo “Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Na. 8 ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa)”ambapo “Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.

Badala yake, Balozi Sefue alisema kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi C. Mwihava atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini hadi uchunguzi dhidi ya Maswi utakapokamilika.

Wakati Maswi akisafishwa na Ikulu katika kashfa hiyo, tayari aliyekuwa waziri wake, Prof. Sospeter Muhongo amejiuzulu tangu 24 Januari 2015, kwa kile alichoeleza kuwa ni kulinda heshima ya serikali.

Mbali na Prof. Muhongo, vigogo wengine waliong’oka kwa kashfa hiyo ya uchotwaji wa Sh. 306 bilioni ni pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.

error: Content is protected !!