June 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la UDA: Serikali yamlinda Salma Kikwete, Ridhwan

Spread the love

SERIKALI imetetea uuzwaji wa hisa za Shirika la Usafirishaji nchini (UDA) kwa Kampuni ya Simon Group na kwamba, kampuni hiyo inamilika hisa hizo kihalali, anaandika Regina Mkonde.

Lawrance Mafuru, Msajiri wa Hazina akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliiuzia UDA hisa kihalali.

Utetezi huo unawapa pumzi Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na Ridhwan Kikwete, mtoto wa rais huyo na Prof. Juma Kapuya, aliyekuwa Mbunge wa Urambo Magharibi ambao wanatajwa kuwa miongoni mwa wana hisa kwenye kampuni hiyo.

“Bodi ya UDA iliyokuwepo muda ule ilikiuka taratibu za uuzaji wa hisa za serikali bila ya Baraza la Mawaziri ambalo lenye mamlaka ya kufanya maamuzi ya uuzwaji wa hisa kuamua kuuza hisa hizo,” amesema Mafuru.

Anaeleza kuwa, Bodi ya UDA iliamua kuuza hisa kwa Kampuni ya Simon Group baada ya kuona shirika hilo linayumba hivyo lilihitaji muwekezaji ili kulifufua.

“Baraza la Mawaziri chini ya mwenyekiti wake ambaye ni rais halikukaa kikao cha kufanya maamuzi ya kuuza hisa na kwamba, baada ya bodi kuona serikali inachelewa kutoa maamuzi ikaamua kuuza hisa za serikali,” anasema.

Amefafanua kuwa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ndilo lililouza hisa zake kupitia Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji hilo kwa kushirikiana na wajumbe wenzake watatu akiwemo Mwanasheria wa Jiji.

“Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na jiji, lilipokea fedha kutoka Kampuni ya SGL kwa ajili ya manunuzi ya hisa zake na kwamba kwa sasa jiji halimiliki UDA, ” amesema.

Amedai, UDA linamilikiwa kihalali na Kampuni ya SGL ambayo inahisa asilimia 51 iliyouzwa na jiji pamoja na serikali ambayo ina hisa ya asilimia 49.

“Aliyeuza hisa za UDA kwa SGL ni Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na wajumbe wengine watatu akiwemo Mwanasheria wa Jiji, sasa kama Masaburi hakuwa Meya halali wa jiji basi hisa hazikuuzwa kwa kampuni ya SGL,” ameeleza.

Akieleza mwanzo wa ugawaji wa hisa za UDA kutoka kwa serikali kwenda Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambapo amesema, serikali iliona bora igawe hisa za asilimia 51 kwa jiji hilo ambalo UDA linapofanya kazi zake.

“Mnamo mwaka 1974 serikali ilianzisha shirika la UDA, mwaka mmoja baadaye serikali iliamua kugawa hisa ya asilimia 51 kwenda kwa jiji la Dar es Salaam na yenyewe kubaki na asilimia 49 ambazo inazo hadi sasa,” amesema.

Hivi karibuni Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam na Baraza la Halmashauri ya Jiji hilo lilikana kuitambua Kampuni ya SGL kuwa, mmiliki halali wa UDA.

Kwa mujibu wa maelezo yao, Masaburi alichukua jukumu la kuuza hisa za jiji kwa Kampuni ya SGL bila kulishirikisha baraza la madiwani la kipindi ambacho uuzaji ulipofanyika.

Siku tatu zilizopita, Saed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo alisema, halmashauri haikuuza UDA licha ya Simon Group Limited kudai kununua.

Kwenye mkutano huo ambao pia uliohudhuriwa na Isaya Mwita Charles, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Kubenea alisema, mkutano uliokabidha UDA kwa Simon Group uliitishwa bila baraka za wenye mali – Baraza la Madiwani la Jiji na Msajili wa Hazina na kwamba, ulihudhuriwa na watu wanne tu.

“Kwanza tunataka mtambue halmashauri haikuuza UDA kwa kuwa, Simon Group Limited wametumia hati ya UDA – mali ya wananchi kufanya biashara. Haturudishi fedha hizi mpaka tufanye hesabu, tujue kampuni hii imepata faida kiasi gani.

“Hata katika mradi wenyewe wa UDA-TR, kumesheheni utapeli. Unaoitwa mkutano mkuu maalum wa wana-hisa wa tarehe 10 Juni 2011, uliosimamiwa na Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji kuidhinisha pamoja na mengine, uuzaji wa hisa za UDA, haukuwa halali,” amesema Kubenea.

Kubenea amesema, mkutano uliokabidha UDA kwa Simon Group uliitishwa bila baraka za wenye mali – Baraza la Madiwani la Jiji na Msajili wa Hazina na kwamba, ulihudhuriwa na watu wanne tu

“Watu hawa ni Dk. Didas Masaburi mwenyewe ambaye alikuwa mwenyekiti; Mkurugenzi wa Simon Group, Robert Kisena ambaye alikuwa katibu; Mwanasheria wa jiji, Isaac Nassor Tasinga na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Phillip Mwakyusa,” amesema Kubenea.

error: Content is protected !!