May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yamjibu Nape kuhusu sakata la korosho

Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imesema italifanyia kazi ombi la kurejesha fedha za tozo ya mauzo ya nje ya nchi (Exporty Levy), ya zao la korosho, kwa wakulima wa zao hilo, ili waweze kumudu gharama za uzalishaji. Anaripoti Nasra Bakari, DMC…(endelea).

Kauli hiyo ilitolewa jana tarehe 25 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma, na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akimjibu Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, aliyeomba Serikali irudishe fedha hizo ili kunusuru zao hilo lisife, kutokana na wakulima kushindwa kumudu gharama za uzalishaji.

Akijibu ombi hilo, Bashe alisema ““niwahakikishie kwamba suala la kuingilia na kuharibu mifumo iliyojengwa vizuri hatuwezi kulirudia hilo jambo, lakini suala la export levy nataka niwahakikishie kwenye Bunge hili, kwamba tunalichukua na tunaenda kulifanyia kazi,” alisema Bashe.

Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama (CCM)

Aidha, Bashe alisema wizara hiyo inaendelea kuweka mazingira mazuri katika kilimo cha korosho, ili kuongeza uzalishaji wake.

“Jambo jingine ambalo limeongelewa na wabunge kwa uchungu mkubwa, nje ya export levy kwenye zao la korosho ni changamoto ya uzalishaji. Sisi kama Wizara ya Kilimo tunaamini mazao haya ya kilimo yana uwezo kujiendesha yenyewe,” alisema Bashe na kuongeza:

“Na takwimu, tathimini uzoefu umeonesha kwamba wakulima wanaweza kujiendesha wenyewe wakijengewa mazingira mazuri na sisi ndiyo kazi yetu.”

Awali, Nape alisema, tangu Serikali ilipofanya mabadiliko katika sheria ya tasnia ya korosho 2018, ambayo yalisababisha fedha zote za tozo ya mauzo ya zao hilo nje ya nchi, kupelekwa katika mfuko mkuu wa fedha za Serikali, badala ya mfuko wa kuendeleza korosho, uzalishaji wa zao hilo umeshuka.

error: Content is protected !!