September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yalifungia Raia Mwema siku 30

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imesitisha leseni ya Gazeti la Raia Mwema, kwa muda wa siku 30 kuanzia kesho tarehe 6 Septemba 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Leseni jiyo imesitishwa leo Jumapili, tarehe 5 Septemba 2021 na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Gerson Msigwa.

“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 9(b) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016 nimeamua kusitisha kwa muda wa siku thelathini (30) leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Raia Mwema kuanzia kesho tarehe 06 Septemba, 2021,” imesema taarifa ya Msigwa.

Taarifa ya Msigwa imedai kuwa, gazeti hilo limesitishiwa leseni yake ya uchapishaji na usambazaji kwa kosa la kukiuka misingi ya maadili ya taaluma ya habari, kwa kufanya upotoshaji.

“Uamuzi wa kusitisha leseni ya gazeti la Raia Mwema unatokana na mwenendo na mtindo wa uandishi wa habari na makala, ambao kwa kiasi kikubwa unakiuka misingi ya maadili ya taaluma ya habari kwa kufanya upotoshaji wa mara kwa mara wa taarifa na uchochezi wa bayana,” imedai taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imedai “kwa kufanya hivyo gazeti hili limekiuka masharti ya leseni liliyopewa jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuleta chuki miongoni mwa jamii na vilevile kuwafanya wananchi waichukie Serikali na viongozi wake.

Taarifa hiyo imetaja habari zinazodaiwa kukiuka misingi na maadili ya uandishi wa habari, ni ‘maumivu mapya 17’ iliyotolewa katika gazeti hilo toleo Na. 844 la tarehe 21 Agosti 2021.

“Katika habari hii gazeti lilikwenda kinyume na vifungu vya 52(1) (a), (c), (d) na (e) pamoja na 54(1) vya Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016 kwa kuchapisha na kusambaza habari zinazoleta taharuki miongoni mwa jamii na wananchi kwa kuonesha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawaletea maumivu wananchi kwa kuweka tozo 17 za kazi mbalimbali za wasanii,” imedai taarifa hiyo.

“Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari inaamini kuwa adhabu hii itawapa nafasi ya kuboresha masuala yanayohusu weledi wa Uandishi wa Habari na utekelezaji wa masuala yote yanayohusu uzingatiaji wa Sheria, kanuni na  maadili ya taaluma ya habari,” imesema taarifa ya Msigwa.

Aidha, taarifa ya Msigwa imesema wamiliki wa gazeti hilo wanaweza kukata rufaa kwa Waziri wa Habar ndani ya siku 30.

“Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016, ikiwa wahusika hawataridhika na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari, wanayo haki ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya Habari ndani ya siku thelathini (30) tangu siku ya uamuzi huu,” imesema taarufa hiyo.

Gazeti hilo ni la pili kupewa adhabu katika uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tangu aapishwe tarehe 19 Machi mwaka huu.

Tarehe 12 Agosti Mwaka huu Gazeti la Uhuru lilipewa adhabu ya kusitishiwa leseni ya uchapishaji kwa muda wa siku 14 baada ya kudaiwa kuandika habari isiyo sahihi kuwa Rais Samia hana nia ya kugombea urais 2025.

error: Content is protected !!