August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siri MSETO kufungiwa zavuja

Spread the love

SERIKALI ya Rais John Magufuli imelifungia Gazeti la MSETO kwa miezi 36 (miaka 3) kwa madai, limeandika habari za uongo, anaandika Regina Mkonde.

Hata hivyo, habari za ndani kutoka katika Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaeleza kuwa, serikali inakerwa na habari za uchambuzi wa kina kuhusu namna Rais Magufuli anavyoendesha nchi.

Katika magazeti ya Tanzania, MSETO ni miongoni mwa magazeti ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuandika habari za uchunguzi na zenye mwelekeo wa kuikosoa serikali kwa maslahi ya umma.

“Mkubwa anakerwa na namna mnavyopekenyua kuhusu serikali yake. Wengine wanalegeza lakini nyingi hamuonekani kulegeza. Tabia hii imekuwa ikimkera,” kimeeleza chanzo chetu cha kila siku ndani ya serikali na kuongeza;

“Mlikuwa mnatafutwa muda mrefu, lakini walikuwa wanaangalia wapi waanzie. Siku hizi mkuu huagiza tu bila hata kutoa sababu za uamuzi wake na mtu lazima afanye kwa kuwa anatetea ugali wake.”

Nape Nnauye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amedai kuwa uamuzi huo umefanywa na serikali ya awamu ya tano kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo.

Nape amewaambia wanahabari kuwa, “Serikali kwa masikitiko makubwa imelazimika kuchukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo wa kuandika na kuchapisha habari ya uongo na kughushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za serikali kwa nia ya kumchafua Rais na viongozi wa serikali.”

Habari iliyoliponza gazeti hilo ni ile ya toleo Na. 480 la tarehe 4 hadi 10 Agosti 2016 ikiwa na nyaraka (barua) kutoka Shirika la Madini la Taifa la (STAMICO) yenye kichwa cha habari; “Waziri Amchafua JPM” Amhusisha na rushwa ya uchaguzi mkuu, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano.

Toleo la gazeti la MSETO lilosababisha kufungiwa
Toleo la gazeti la MSETO lilosababisha kufungiwa

Barua hiyo inaonyesha kuwa Serikali kupitia kwa Mhandisi Edwin Ngonyani Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakati huo akiwa Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa STAMICO iliandika barua ya kushukuru kupokea fedha zaidi ya dola za kimarekani 65,000 kwa ajili kampeni kutoka kwa mwekezaji James Sinclair.

Serikali imefanya maamuzi ya kulifungia gazeti la MSETO kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 kifungu cha 25(1) ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wanahabari kwa zaidi ya miongo minne sasa, sheria hiyo inatajwa kuwa ni kandamizi kwa vyombo vya habari.

Wanahabari wamekuwa wakipendekeza sheria hiyo inayompa mamlaka Waziri anayeshughulikia masuala ya habari kukifungia chombo chochote cha habari iwapo, kwa mtazamo wake binafsi ataona chombo hizo hakizingatii maslahi ya umma. Hakuna ufafanuzi juu ya neon ‘maslahi ya umma’ na kipimo chake.

Sheria hiyo inatamka katika kifungu cha 25(1); “Waziri akiona kwamba kwa ajili ya maslahi ya umma au kwa ajili ya kudumisha amani na usalama, aweza kutoa amri na kutangaza kwenye gazeti la serikali ambayo itaeleza kwamba gazeti lililotajwa katika amri hiyo litasitisha kutolewa tangu siku itakayotajwa katika amri hiyo.”

Aidha serikali pia imetangaza kusitisha uchapishwaji wa gazeti la MSETO kuchapishwa katika njia nyingine zote za upashanaji habari ikiwemo mitandao. Uamuzi huu umetangazwa kufanywa kwa kutumia Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta sura ya 306.

Hili ni gazeti la pili kufungwa na Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miezi saba, ambapo Januari mwaka huu serikali ilitangaza kulifutia usajili kabisa gazeti la MAWIO kwa madai ya kuandika habari za uchochezi kwa muda mrefu.

error: Content is protected !!