MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imetupilia mbali mapingamizi ya Serikali, katika kesi Na. 16/2021, iliyofunguliwa na Alexandra Bakunguza, kupinga elimu ya juu kutolewa kwa malipo. Anaripoti Noela Shila, TUDARCo … (endelea).
Mapingamizi hayo yalitupwa na mahakama hiyo, jana Jumanne tarehe 17 Agosti 2021, mbele ya Jaji Modesta Opiyo.
Serikali iliwasilisha mapingamizi matatu katika kesi iliyofunguliwa na mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (TUMa), jijini Arusha, tarehe 29 Julai 2021kwa madai kwamba haina mashiko.
Jaji Opiyo alikataa mapingamizi hayo, akidai kwamba yanaingia kwenye kiini cha msingi wa kesi, kinyume cha mapingamizi ya awali yanavyopaswa kufanyika.
Kufuatia hatua hiyo, mahakama hiyo itaendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo, ambapo imepanga kuisikiliza tarehe 2 Septemba 2021.
Bakunguza amefungua kesi hiyo, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Mhitimu huyo wa chuo kikuu, anaomba wanafunzi wasilipishwe gharama za masomo ya elimu ya juu, badala yake Serikali ibebe jukumu hilo.
Katika kesi hiyo, anapinga elimu ya juu kugharamiwa na Serikali kwa njia ya mkopo, kinyume na Ibara ya 11 ya katiba ya Tanzania, ambayo inayoelekeza Seriali itoe elimu na mafunzo ya ufundi kwenye ngazi zote kwa usawa.
Leave a comment