August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yakiri uhaba wa fedha

Spread the love

SERIKALI imesema, kutokana na uwezo mdogo wa kifedha haitaweza kuchukua vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), anaandika Dany Tibason.

Hayo yameelezwa leo Bungeni na Dk. Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vitimaalum, Munira Khatib(CCM).

Mbunge huyo alitaka kujua ni kwanini serikali isianzishe mpango maalum wa kuwapeleka  vijana wanaomaliza kidato cha nne nchini JKT ili wakimaliza mafunzo waweze kujiajiri wenyewe pamoja na kuwa wazalendo.

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la vijana wanaomaliza kidato cha nne na ongezeko la shule za Kata nchini vijana hawa wamekuwa wakizagaa mitaani bila kujua la kufanya na matokeo yake kujiingiza kwenye vitendo hatarishi kama dawa za kulevya, uvutaji wa bangi, wizi, udokozi,” amehoji mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Dk. Mwinyi alisema utaratibu uliopo hivi sasa wa vijana kujiunga na Jeshi hilo ni ule wa vijana wa kujitolea ambao ni wenye elimu kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu.

Sambamba na hilo amesema pia utaratibu mwingine ni wa mujibu wa sheria ambao ni kwa vijana waliomaliza kidato cha sita.

Dk. Mwinyi amesema hivi sasa uwezo wa JKT kuchukua vijana wa kujitolea ni kati ya vijana 5000 hadi 7000 kwa mwaka kutokana na bajeti inayotolewa.

Aidha amesema ushauri wa mbunge huyo ni mzuri na serikali itafanya maandalizi ya kambi nyingi zaidi na kutenga bajeti kubwa zaidi kwaajili ya uendeshaji kadri ya uwezo wa kifedha utakavyoruhusu.

error: Content is protected !!