July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yakataa deni la walimu

Spread the love

SERIKALI imebaini wizi na udanganyifu uliofanywa na walimu na wakurugenzi wa Halmashauri katika kuandaa madai ya walimu ya mwaka 2014. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Wizi na udanganyifu uliogundulika ni walimu kujibadilisha majina, walimu hewa, kudai madeni ambayo yalishalipwa pamoja na wengine kutoa taarifa zisizosahihi.

Madai hayo ya walimu yalipitiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ndipo Wizara ya Fedha kupitia idara ya Mkaguzi wa ndani Mkuu wa Serikali iliamua kufanya uchambuzi ili kujiridhisha na madai yaliyowasilishwa kuna mapungufu mengi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile amesema uchambuzi huo ulifanywa na wakaguzi wa ndani wa mamlaka ya serikali za mitaa na timu ya wakaguzi wa ndani chini ya usimamizi.

Amesema mara baada ya kufanyika uchambuzi walibaini kuwa madai yalitolewa na walimu dhidi ya serikali ya Sh. 19.6 bilioni hayakuwa sahihi bali yenye usahihi ni Sh. 5.7 bilioni.

Likwelile amesema katika madai hayo kulionekana baadhi ya walimu kujipandisha vyeo, kujiongezea majukumu, na wengine kutumia majina mawili tofauti huku akiwa ni mtu mmoja ili apate fedha nyingi.

“Bila sisi kulisimamia hilo na kufanya uchambuzi serikali ingeweza kuingia katika hasara kubwa sana kwani wasimamizi wa kuaandaa madai hayo hawapo makini. Pia tulibaini kuna walimu hewa kwamaana hiyo Halmashauri iliandika madai ya walimu hewa,” amesema Likwelile.

Mbali na hilo, Likwelile amesema alishangazwa sana na kitendo cha Rais wa Walimu, Gratian Mukoba kutangazia umma kuwa walimu wanaidai serikali kiasi hicho cha fedha wakati walishalipwa kiasi halali cha fedha kilichofanyiwa uchambuzi.

“Deni lao la mwaka 2014 tumeshawalipa, kinachusubiliwa sasa ni madeni ya mwaka huu, na tayari yanafanyiwa kazi na Tamisemi kisha yaje huku kufanyiwa uchambuzi wa mwisho”

“Safari hii kila kitu kinafanyika Tamisemi ili madeni yakija huku yakibainika kuwa na kasoro kama hizi za sasa tutawabana wao pamoja na waandaaji wa chini sheria zitafata mkondo wake,” amesema Likwelile.

Likwelile ametoa wito kwa waalimu kuwa makini katika kutoa taarifa zao na wasikubali kutumiwa na viongozi wao ili kujinufaisha binafsi, kwani serikali ipo tayari kulipa madeni yote baada ya kufanyiwa uchambuzi na kuwa na uhakika nayo.

error: Content is protected !!