SERIKALI ya Tanzania imekamikisha rasimu ya marekebisho ya sera ya elimu, ambayo hivi karibuni itatolewa ili wadau kutoa maoni kwa ajili ya kuiboresha zaidi kabla haijaanza kufanya kazi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Hayo yameelezwa leo Jumapili, tarehe 6 Novemba 2022 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda, katika mahafali ya wanafunzi wa kidato cha nne kutoka shule 11 za sekondari za kiislamu, zinàzosimamiwa na Taasisi ya Islamic Development Foundation (IDF) jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa shule hizo ni, Ilala Islamic, Alharamain Islamic, Dar es Salaam Islamic, Kunduchi Girls Islamic, Kibraten Islamic, Ununio Boys Islamic, Nuru Islamic, Temeke Islamic na Kinondoni Muslim.
Prof. Mkenda amesema sera hiyo itaanza kutumika 2024, kama mchakato wa kuupitisha utakamilika 2023.
“Rasimu ya sera imekamilika, baada ya hapo tutaitoa kwa ajili ya mjadala. Mapendekezo yapo katika marekebisho makubwa kwenye mfumo wa elimu. Sasa tunakamilisha mchakato wa ndani, mwakani ni mchakato wa maamuzi na mwaka unaofuata kuanza utekelezaji,” amesema Prof. Mkenda.
Waziri huyo wa elimu amesema, marekebisho hayo yatazingatia namna ya kuweka miongozo ya kuimarisha maadili kwa wanafunzi, huku akiwataka viongozi wa dini watoe mapendekezo yao kuhusu suala hilo muda utakapofika.
Aidha, Profesa Mkenda amesema wizara yake italifanyia kazi ombi la mwakilishi wa wamiliki wa shule hizo, Maulid Mtulia la masharti ya kuomba vibali vya usajili wa shule binafsi yapunguzwe, ili kutoa nafasi kwa watu wengi kuzifungua.
Akizungumzia mahafali hayo, Prof. Mkenda amezipongeza shule hizo kwa kuboresha elimu wanayotoa, kitendo kilichpandisha hadhi kwa shule za kiislam nchini.
Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salim, amewataka wanaohitimu kuendelea kufuata maadili kama dini ya Kiislam inavyowaelekeza.
“Serikali yetu inategemea kuwoana kuwa mna maadili. Ndio maana waziri yuko hapa anauchungu kuona maadili yanamomonyoka. Ukitazama matukio mabaya basi majina ya kiislamu ni mengi kuliko wenzetu. Lazima tuhakikishe maadili ndiyo kila kitu, pasina maadili hakuna kitu,” amesema Sheik Mussa.
Mwenyekiti wa Shule za Kiislamu Tanzania, Mwinyikombo Ayub, amesema shule hizo zitaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuhakikisha zinatoa elimu bora Kwa wanafunzi, hususan ya dini ili kukabiliana na changamoto za mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Mwakilishi wa Wakuu wa shule hizo, ambaye ni Mkuu wa Shule ya Alharamain Islamic, Buhero Issa Buhero, akitaja maendeleo ya shule hizo amesema zinaendeshwa kufuata kanuni na miongozo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Buhero amesema matokeo ya shule hizo katika mitihani ya taifa, yanaridhisha kwani waliohitimu 2021 walikuwa zaidi ya 500 na waliofaulu ni 501 kujiunga na elimu ya kidato cha tano na sita pamoja na vyuo vya elimi ya juu na kati.
Amesema, 2021 kulikuwa na wahitimu wa 182 wa kidato cha tano na sita, ambapo wote walifaulu na kupata nafasi ya kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.
Aidha, Buhero ametaiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuweka miongozo itakayosaidia kuwa na walimu wa masoko ya dini wanakuwa wa kudumu, ili kusaidia wananchi kupata elimu ya dini na kuwa na maadili mema.
Leave a comment