May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yakamata madini ya Sh. 501 Mil. yakitoroshwa

Madini ya dhahabu

Spread the love

 

SERIKALI imesema imefanikiwa kukamata madini ya Sh 501.2 milioni katika matukio ya utoroshaji katika kipindi cha kati ya Julai 2021 hadi Machi 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hayo yameelezwa bungeni leo Ijumaa tarehe 29 Aprili 2022 na Waziri wa Madini, Doto Biteko, akisoma hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Biteko amesema madini hayo yakiwemo dhahabu, vito, mchanga na madini ya viwandani yalikamatwa katika matukio ya utoroshaji na biashara haramu ya madini katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Manyara, Dodoma, Lindi, Geita, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza.

Amesema imefanikiwa kukamata madini hayo baada ya kuimarisha usimamizi na ukaguzi kwenye maeneo ya uchimbaji, mipaka ya nchi pamoja na kuanzisha na kuimarisha masoko na vituo vya uuzaji wa madini.

Waziri huyo amesema kazi ya ukamataji hufanywa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Ofisi ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya pamoja na raia wema.

“Kutokana na juhudi hizo kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi, 2022 shilingi bilioni 461.6 zimekusanywa na kuwasilishwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ikilinganishwa na shilingi bilioni 445.2 zillizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021, sawa na ongezeko la asilimia 4,” amesema.

error: Content is protected !!