August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yajitoa kesi ya kada wa CCM

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachilia huru Thomas Ngawaiya, aliyekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), baada ya Serikali kuiondoa kesi iliyokuwa ikimkabili ya kujenga hoteli yenye thamani ya Sh. 500 milioni  kwa kutumia Wakandarasi wasiosajiliwa, anaandika Faki Sosi.

Hatua hiyo ilifikiwa jana mahakamani hapo, mbele ya Respicius Mwijage, Hakimu Mkazi Mkuu, baada ya Mwendesha Mashtaka wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (ERB), Saddy Kambona kuiomba mahakama hiyo kuindoa kesi hiyo chini ya Kifungu cha 98 (a) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Baada ya Kambona kuwasilisha ombi hilo, Hakimu Mwijage alikubaliana na ombi hilo na kuiondoa kesi hiyo kutokana na kifungu cha sheria kilichoombwa na upande huo kuliondoa shauri hilo.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Ngawaiya kuwasilisha mahakamani hapo, kibali cha ujenzi wa jengo hilo na kibali cha wakandarasi hao.

Ngawaiya ambaye ni kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa anatuhumiwa kutenda kosa la kuagiza ujenzi wa jengo la hoteli, kwa wakandarasi wasiosajiliwa na ERB.

Ilidaiwa kuwa jengo hilo, lipo kiwanja namba 32, makutano ya mitaa wa Dosi na Wazani, eneo la Magomeni Mapipa, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo anatuhumiwa kutenda kosa hilo kinyume na sheria ya bodi hiyo.

Awali Ngawaiya aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wazee wa CCM mkoani Kilimanjaro, alikuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya sh. 250 milioni, kila mmoja akiwasilisha mahakamani hapo hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

 

error: Content is protected !!