January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yajitetea bei ya tumbaku

Spread the love

SERIKALI imesema, haihusiki kupanga bei ya tumbaku na badala yake hupangwa na wadau wenyewe kadri wanavyoona inafaa. Anaandika Danny Tibason.

William Tate Ole Nashe ambaye ni Naibu Wazili wa Kilimo Mifugo na Uvuvi ametoa kauli hiyo leo bungeni akijibu swali la Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo (CCM).

Sitta alitaka kujua kama serikali ina mpango wa kupanga bei ya tumbaku ili kuwasaidia wakumlima ambao wanaonekana kutumia nguvu kubwa katika kilimo hicho na kuuza mazao yao kwa bei ya chini.

Mbunge huyo wa Urambo amesema, wakulima wa tumbaku hutumia muda na fedha nyingi lakini wanapofikia hatua ya kuuza tumbaku, huuzwa kwa bei ndogo jambo ambalo huwakatisha tamaa.

“Mfumo wa sasa wa kuwahudumia wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Urambo na Mkoa wa Tabora kwa ujumla una mapungufu mengi yanayowaletea wakulima usumbufu kama vile bei za pembejeo kuwa kubwa kutokana na kuagizwa kutoka nje na riba kubwa za benki.

“Masoko ya bei ya tumbaku kutokuwa na uhakika na hatimaye kushuka kwa thamani ya tumbaku. Je ni kwanini hasara inayotokana na matatizo hayo ibebwe na wakulima peke yake? Je serikali imejipanga vipi kuondoa matatizo hayo ili mkulima wa tumbaku anufaike na kilimo na hatimaye ajikwamue kiuchumi?” amehoji Sitta.

Waziri Ole Nashe amesema, serikali haina mpango wowote wa kupanga bei ya zao la tumbaku isipokuwa wadau na wakulima ndio walio na jukumu hilo na kwamba, serikali inaendelea kuchukua changamoto za wakulima hao na kuangalia namna ya kuzitatua.

Alisema hatua hizo ni pamoja na kuboresha mfumo wa upangaji wa bei ya tumbaku ambapo wakulima hupendekeza bei yenye tija kwao na kuiwasilisha kwa wanunuzi kupitia katika vikao vya halmashauri ya tumbaku.

error: Content is protected !!