July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yajipanga kurudisha mitaala ya michezo mashuleni

Spread the love

SERIKALI imeahidi kurejesha mitaala ya michezo katika shule za msingi na sekondari, viwanja vya michezo, kuongeza bajeti ya michezo pamoja na kupunguza kodi kwa vifaa vya michezo vinavyotoka nje ili kuiendeleza sekta ya michezo nchini, anaandika Regina Mkonde.

Ahadi hiyo imetolewa leo na Jenista Mhagama, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu) katika Tamasha la Michezo la Wanawake, lililoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

“Serikali itahakikisha inaondoa changamoto ya viwanja kwa kushirikiana na wizara ya ardhi, inaongeza bajeti ya michezo, kusajiri vyama vingi vya michezo na kupunguza ama kuondoa kodi kwa vyama vya michezo vitakavyoingiza vifaa vya michezo nchini kutoka nje,” amesema Mhagama.

Mhagama amesema sekta ya michezo iikihimarika itahamasisha wanawake kushiriki kwenye michezo na kwamba itawasaidia kujiajiri na kupata maendeleo kupitia michezo.

“Sekta ya michezo ikihimarika itasaidia wanawake kujiajiri kupitia michezo na kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia michezo,” amesema Mhagama.

Waziri Jenista amezitoa ahadi hizo kwa niaba ya Makamo wa Rais Mama Samia Suluhu, baada ya BMT kuiomba serikali kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya michezo nchini.

Zainab Matitu Vulu, Makamo Mwenyekiti wa BMT amesema kuwa, sekta ya michezo nchini imezidi kudumaa kutokana na uhaba wa fedha, vifaa vya michezo kutoka nje kutozwa kodi kubwa, na viwanja vya michezo kuwa chakavu.

“Serikali hutenga bajeti ndogo isiyokidhi mahitaji ya michezo hali inayochangia sekta ya michezo kudumaa, pamoja na utozwaji wa kodi kubwa kwa vifaa vya micehzo vinavyoingia nchini kutoka nje,” amesema Vulu.

error: Content is protected !!