July 24, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yajikanganya kuhusu misaada ya MCC

Spread the love

SIKU mbili tangu Marekani iifutie Tanzania misaada kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia, viongozi wa serikali ya Tanzania wamekuwa na misimamo inayojikanganya, anaandika Happiness Lidwino.

Wakati Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango,  na Dk Servacius Likwelile, Katibu Mkuu wa wizara hiyo,  wakisema pesa za MCC hazikuwekwa kwenye bajeti sababu walijipanga baada ya kuona dalili nyingi za kuzikosa, Balozi Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, amesononeka kwa Tanzania kukosa msaada wa MCC.

Balozi Mahiga aliwaambia waandishi wa habari wiki hii Jijini Dar es Salaam kuwa, hatua ya MCC inafuta imani na uelewano uliokuwepo kati ya Tanzania na wahisani.

Alisema: “Suala la nishati ndio mradi wa maendeleo ya nchi hii, hatuwezi kufanikiwa kwa chochote bila kuwa na nishati ya umeme, mfano ukienda hospitalini vifaa vingi vinahitaji umeme, au shuleni.

“Wametufutia msaada pale ambapo maendeleo yetu yanaanzia, na ni eneo ambalo linauma zaidi, wametuahidi pesa kisha wakaziondoa.”

Kauli ya Mahiga imepingana pia na ya Dk Lutengano Mwakahesya, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA), ambaye ametamba kuwa REA haitaathirika kwani hakuna msaada wala pesa yoyote wanayoitegemea kutoka  MCC.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwakahesya amesema REA inategemea asilimia 90 kutoka serikalini na asilimia 10 kutoka kwa wahisani. Amedai kwamba serikali haijawahi kupokea msaada kutoka MCC tangu mradi huo uanze mwaka 2007.

Amesema wafadhili wanaochangia REA ni asilimia tatu (3%) na kiasi kingine cha pesa hutoka Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco).

“Wasambazaji na wazalishaji, hupata Tsh.100 kutoka  kwenye  mafuta ya petrol, na Tsh.150  kwenye mafuta ya taa na wahisani kutoka nje, lakini si MCC,” amesema  Mwakahesya.

Ameongeza kuwa sheria ya nishati ya vijiji inasema mzalishaji yeyote anatakiwa kuchangia REA asilimia tatu  na wanapata asilimia hizo kutoka kwa wazalishaji na wasambazaji.

Dk. Mwakahesya amesema  tathimini ya usambazaji wa mradi wa umeme vijijini hadi sasa inaonesha kuwa wamesambaza  umeme huo kwa vijiji 5200, sawa na asilimia 36.

Amedai nchi nzima ina vijiji 15,000 na umeme umefanikiwa kufika vijiji hivyo,  na bado wanaendelea  na kazi hiyo.

Wakati mradi huu unaanza mwaka 2007 usambazaji wa umeme vijijni ulikuwa ni kwa asilimia mbili. Wizara inadai kuwa sasa umefikia asilimia 36.

Dk. Mwakahesya amesema kwamba mradi huo unakua na serikali itafikia malengo ya kusambaza umeme katika vijiji vyote kama ilivyopanga. Anadai hadi sasa imejenga transfoma 5000 nchi nzima bila kutegemea msaada wa MCC.

Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa hadi Tanzania inafutiwa awamu ya pili ya msaada huo mwanzoni mwa wiki hii, MCC ilikuwa imetoa Tsh. trilioni 1.18 katika awamu ya kwanza.

Fedha hizo, pamoja na mambo mengine, zilitumika kutengeneza mtandao wa kilomita 3,000 za nyaya za umeme vijijini, na kilomita 450 za barabara za lami ikiwamo ile ya Tunduma – Sumbawanga, yenye zaidi ya kilomita 240.

Awamu ya pili ya fedha hizo ilitarajiwa kuendeleza miradi ya umeme vijijini na kujenga barabara za lami katika mikoa inayozalisha kwa wingi vyakula na kuunganisha na maeneo mengine ya nchi, ili wakulima waweze kuuza mazao yao.

Tarehe 29 Septemba mwaka jana wakati akiwa mgombea urais, John Magufuli, akiwa katika Kata ya Mvumi, Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, alisema anawashangaa watu wanaokejeli safari za aliyekuwa Rais Jakaya Kikwete kwenda nchi za nje, akisema zimeleta manufaa makubwa kwa taifa.

Miongoni mwa faida ambazo Magufuli alisema zimetokana na safari za Rais Kikwete ni Tsh. bilioni 992 zilizotolewa na Serikali ya Marekani kupitia mfuko wa MCC kwa ajili ya miradi ya umeme kama sehemu ya matunda ya safari za Rais Kikwete nchi za nje.

Alisema: “mabilioni yaliyotolewa na MCC, yatasaidia kusambaza umeme katika mikoa na vijiji vingi nchini na tayari mipango imekamilika ya kuwafikishia wananchi nishati hiyo.”

error: Content is protected !!