July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yajibu jeuri waliobomolewa

Spread the love

SERIKALI imegoma kuwapa viwanja wananchi waliobomolewa nyumba zao zilizokuwa bondeni kwa madai jiji limejaa na hakuna viwanja, anaandika Regina Mkonde.

Said Mecky Sadick, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema hayo leo jijini Dar es Salaam katika kikao cha kwanza cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dar es Salaam.

Hivi karibuni serikali iliendesha bomoabomoa kwenye maeneo ya bondeni hususan katika Mbonde la Mkwajuni na kusababisha vifo na mateso kwa baadhi ya wakazi hao.

Bona Kaluwa, Mbunge wa Jimbo la Segerea na Abdallah Mtulia Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, walizuia kuendelea kwa bomoabomoa hiyo kupitia Mahakama.

“Wakazi wa Kinondoni waache jeuri, wanajua fika kuwa wamejenga sehemu zisizostahili, wamebomolewa lakini wamerudisha vibanda na kuendelea kuishi na kusema serikali inawaonea,” amesema Sadick na kuongeza;

“Serikali haiwezi kuwapa ardhi waliobolewa, kwanza ardhi hakuna katika Jiji la Dar es Salaam, halafu unamsaidiaje mtu aliyevunja kisheria?” amesema.

Sadick amesema kuwa, serikali haikuwapeleka maeneo hayo na kwamba haina sababu ya kuingia gharama kuwapa viwanja.

Katika mkutano huo Bona aliitaka serikali kuwapa viwanja waathirika kama ilivyofanya mwaka 2012 ambapo wananchi walipewa viwanja Mabwepande.

“Serikali ilichangia kuongeza kasi ya ujenzi wa mabondeni sababu, ili ruhusu huduma za kijamii kupelekwa katika maeneo hayo kama shule, barabara na hospitali na iliwapa moyo kuendelea kujenga katika maeneo hayo,” amesema Bona.

Mtolea amesema kuwa, wananchi waliojenga vibanda katika Bonde la Mkwajuni siyo jeuri kama alivyosema Sadick na kwamba hali ngumu ya maisha ndiyo iliyosababisha kujenga eneo hilo.

“Waliojenga vibanda siyo jeuri, hali ngumu ya maisha ndiyo inayosababisha wasihame kwasababu hawana mahali pa kwenda,” amesema Mtulia.

error: Content is protected !!