September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yaitaja vita Ukreinia-Urusi vihatarishi bajeti 2022/23

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania

Spread the love

VITA inayoendelea baina ya Ukreinia na Urusi, imetajwa miongoni mwa vihatarishi kwa utekelezaji wa bajeti ya Serikali 2022/23. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hayo yamebainishwa katika taarifa ya Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2022/23 iliyotolewa leo tarehe 11 Machi 2022.

Serikali imesema katika taarifa hiyo kuwa “vihatarishi vya bajeti vinaweza kupunguza au kuongeza mapato na matumizi ya Serikali.”

“Hivi karibuni kumekuwa na vita kati ya nchi ya Urusi na Ukraine ambavyo vimeanza kuonesha athari katika uchumi wa dunia kutokana na baadhi ya bidhaa hususan mafuta kupanda bei,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, imeelezwa kutokana na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa kwa nchi ya Urusi, athari kubwa zaidi zinaweza kujitokeza “kama vita hiyo itachukua muda mrefu.”

Imebainisha kuwa maeneo ya moja kwa moja ambayo yanaweza kuathirika ni pamoja na nishati ya gesi ambapo Urusi ni msambazaji mkubwa wa nishati hiyo kwa takribani asilimia 40.

“Kwa kuwa nchi za ulaya ambazo zimekuwa zikipata nishati hiyo kutoka Urusi zitahamia kwenye nchi nyingine, nishati hiyo inatarajiwa kupanda bei na hivyo Tanzania nayo itaathirika na ongezeko hilo,” imeeleza taarifa hiyo.

Vilevile, maeneo mengine yatakayoathirika ni riba na bei za hatifungani katika masoko ya kimataifa na bei za dhahabu.

“Kwa kuzingatia kuwa Urusi imefungiwa kutumia mfumo wa mawasiliano ya kibenki wa kutuma fedha, biashara kati ya Urusi na nchi nyingine itaathirika ikiwa ni pamoja na utalii, elimu na kugharamia ofisi za ubalozi kwa upande wa Tanzania,” imeeleza zaidi taarifa hiyo na kuongeza:

“Kwa ujumla kuna uwezekano mkubwa wa mfumuko wa bei kuongezeka iwapo vita hivi vitachukua muda mrefu na hivyo kuathiri utekelezaji wa bajeti ya Serikali,”

Vihatarishi vingine vilivyobainishwa na Serikali ni mabadiliko ya tabianchi; mabadiliko ya teknolojia ya biashara (biashara mtandaoni); majanga ya asili na vita; mabadiliko ya viwango vya riba katika masoko ya fedha; mitikisiko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii duniani; na udukuzi wa mifumo ya fedha.

error: Content is protected !!