December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yaipongeza St Anne Marie kwa kutochuja wanafunzi, Yaahidi kuendelea kuongoza Dar/kitaifa

Wanafunzi wa shule ya sekondari St Anne Marie Academy wakiwa kwenye foleni ya kuchukua vyeti vyao kwa mgeni rasmi wakati wa mahafali ya 18 shuleni hapo Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam.

Spread the love

 

SERIKALI imepongeza shule ambazo hazina kawaida ya kuchuja wanafunzi unapofikia muda wa mitihani ya kitaifa iiwemo St Anne Marie Academy . Mwandishi Wetu

Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Kamishna wa Elimu, Dk.Lyabwene Mtahabwa, ambaye alimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda, kwenye mahafali ya 18 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari St Anne Marie Academy ya Mbezi kwa Msuguri.

Alikemea tabia ya ubaguzi unaofanywa na baadhi ya shule kwa lengo la kuongeza ufaulu kwenye mitihani ya kitaifa jambo ambalo alisema ni ubaguzi mkubwa.

“Mheshimiwa Rweikiza Mungu akubariki maana hapa hakuna tabia ya kubagua wanafunzi wakati wa mitihani ya kitaif. Kumbagua mwanafunzi kwa uwezo wake ni kwenda kinyume na haki za watoto,” alisema

Aidha, alisema hatua ya kubagua wanafunzi wakati wa mitihani ya kitaifa ni ukatili mkubwa na fedheha kwa wazazi ambao wamejinyima na kutumia fedha nyingi kuhakikisha mtoto wao anapata elimu bora.

“Badala ya kuwatenga wanafunzi wakati wa mitihani walimu wanapaswa kuwa na mbinu mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wote wanakuwa mahiri kwenye masomo. Watu wanatofautiana uelewa wengine wanaelewa haraka wengine taratibu kwa hiyo mbinu zinahitajika kuwawezesha wote kufaulu,”alisema

Mkurugenzi wa shule ya St Anne Marie Academy, Dk. Jasson Rweikiza akizungumza kwenye mahafali ya 18 ya shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam.

Aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa ubunifu mkubwa walioonyesha wa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama sabuni hali ambayo itawawezesha kuwa wajasiriamali baada ya masomo yao.

“Nimefurahishwa sana na ubunifu wa watoto hapa na wengine wa darasa la tano wamemudu kutengeneza sabuni ambayo kwa kweli nimeifurahia nitaipeleka nyumbani kumwonyesha mke wangu aone kazi za wanafunzi,” alisema

Aliwataka wazazi wawafundishe watoto wao ujasiriamali kama njia ya kujitafutia kipato siku zijazo huku akiwataka wenye shule kufundisha lugha mbalimbali ikiwemo kichina,kiarabu na kifaransa kwani yana soko kubwa.

“Dunia inakwenda kwa kasi sana  nimeona wanafunzi wanazungumza hata kifaransa naomba shule nyingine ziige kwa kuweka lugha mbalimbali kwasababu dunia ya sasa ya utandawazi ukiwa na lugha nyingi umejifungulia milango ya mafanikio ukijifungia kwa kingereza na kiswahili pekee umejiandalia anguko,” alisema

“Mheshimiwa Rweikiza panua wigo wa lugha mbali na Kiswahili, Kingereza na Kifaransa weka lugha zingine kichina na kiarabu ili uweze kupambana kwenye kanda na kwenye jumuiya ya kimataifa dunia inakwenda kwa kasi sana,” alisema

“Aprili mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza tupitie mitaala na mfumo mzima wa elimu ili kuwa na mfumo unaomwandaa mwanafunzi aweze kusimama mwenyewe kujitegemea anapomaliza shule badala ya kukaa nyumbani na kulalamika kwamba hana ajira,” alisema

Kamishna wa Elimu, Dk.Lyabwene Mtahabwa, ambaye alimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda, kwenye mahafali ya 18 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari St Anne Marie Academy ya Mbezi kwa Msuguri akigawa vyeti kwa wahitimu.

Alisema mfumo wa elimu unapaswa kumwandaa mwanafunzi anapomaliza elimu awe na uwezo wa kujiajiri badala ya kupoteza muda kutafuta ajira.

“Tuandae watu wenye uwzo wa kufumbua macho na kuona fursa mbalimbali mhitimu usitegemee kalamu na karatasi pekee yake kama ni kushona shona, kusindika, kufuma, kusuka, kuchomelea, uashi na ujuzi mbalimbali

“Tangu Rais wetu atoe tamko tumeendelea na mchakato wa kupitia mitaala na lengo letu ni kwamba mitaala hiyo ianze kutumika Januari 2024,” alisema

Mkuu wa shule hiyo, Gladius Ndyetabura alisema wanafunzi hao wameandaliwa vizuri na watafanya maajabu kwenye mituhani yao ya mwisho.

Alisma shule hiyo itaendelea kuongoza kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Ubungo na kuingia kwenye kumi bora kitaifa kaama ilivyo kawaida yake.

Alisema shule hiyo imekuwa ikifanikiwa kuingia 10 bora kitaifa kwenye matokeo ya kitaifa na kuwa ya kwanza Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Ubungo kutokana na maandalizi mazuri kwa wanafunzi wake.

“Mazingira yetu ni mazuri na watoto hapa wanakula chakula kizuri ikiwemo pilau mara nyingi tu na huwa tunawapeleka mbuga za wanyama kama motisha ya kufanya vizuri,” alisema Ndyetabura

error: Content is protected !!