August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yahangaika na somo la hisabati

Spread the love

SERIKAL inatarajia kufanya utafiti wa ndani wenye lengo la kuchambua somo la hisabati na kuangalia namna ya kulifanya kuwa rafiki kwa wanafunzi, anaandika Happyness Lidwino.

Utafiti huo unatarajiwa kufanywa kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya chuo kikuu kwa lengo la kuangalia namna gani ya kulifanya somo la hisabati kuwa somo lenye kufanya vizuri nchini.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Pai kitaifa, Paulina Mkonongo, Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, amesema kuwa utafiti huo utahusisha wadau mbalimbali wa elimu katika ngazi zote za elimu pamoja na wanafunzi.

“Tufahamu suala la utafiti ndilo litakalotupa jibu kwanini somo la hisabati limeonekana kuwa bado ni tatizo kwa wanafunzi wetu, hivyo tutajipanga kufanya utafiti huo ambao utahusisha wadau mbalimbali hata wazazi na walimu wenyewe,

“Matokeo ya utafiti wa jumla ulionyesha mwaka jana hisabati hatukufanya vizuri, lakini ili tuweze kufanya vizuri katika somo la hisabati ni lazima wanafunzi wawe na utayari wa kujifunza somo hilo, kumekuwa na uwoga hata kwa baadhi ya walimu wanaofundisha somo hilo, wazazi na hata wanafunzi wenyewe kuwa somo hilo ni gumu lakini mbinu stahiki ya kujifunza na kufaulu somo hilo ni kuwa na utayari wa kujifunza” amesema Mkonongo.

Aidha Mkonongo amesema serikali imejipanga kuhakikisha inaongeza idadi ya walimu wa hisabati nchini kwa lengo la kuondoa changamoto hiyo ambayo imekuwa ni tatizo karibu katika kila shule nchini.

Akizungumzia kuhusu siku ya Pai kitaifa, Mkurugenzi huyo amesema lengo la siku hiyo ni kuikumbusha jamii na serikali kuwa somo la hisabati linahitaji kupewa kipaumbele cha kipekee kutokana na umuhimu wake sambamab na kutafakari mafanikio na changamoto mbalimbali katika ufundishaji na ujifunzaji wa hisabati.

“Tumeungana hapa na chama cha hisabati Tanzania (CHAHITA) kwa lengo la kukumbushana na kuifahamisha jamii kwa kupaza sauti kuwa hisabati ni muhimu; unaona kauli mbiu ya mwaka huu inasema Hisabati ni msingi wa Sayansi na Teknolojia ambapo kauli hii inalenga kuwashawishi vijana kutambua msingi wa sayansi na teknolojia ni somo la hisabati” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA), Said Simba, amesema serikali inatakiwa kutoa vipaumbele kwa walimu ambao walishastaafu kupata nafasi ya kufundisha somo hilo kwa shule ambazo zina upungufu mkubwa wa walimu wa hisabati na kuongeza kuwa tamisemi inasimamia uwepo wa klabu za Hisabati na sayansi kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo hayo.

error: Content is protected !!