September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yafuta leseni ya Gazeti la Tanzania Daima

Spread the love

GAZETI la kila siku la Tanzania Daima, linalomilikiwa na Kampuni ya Free Media Limited, limeingia kifungoni kwa muda usiojulikana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Leo Jumanne tarehe 23 Juni 2020, Patrick Kipangula, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, ametangaza kusitishwa leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo, kuanzia kesho Jumatano tarehe 24 Juni 2020.

Kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa umma, Kipangula amesema, hatua hiyo imetokana na idara hiyo kusitisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa Gazeti la Tanzania Daima, kutokana na kukiuka maadili ya uandishi wa habari.

Kipangula amedai, uamuzi huo umechukuliwa baada ya wahariri wa gazeti hilo kukiuka masharti ya leseni waliyopewa, licha ya kuonywa mara kadhaa.

“Umma unataarifiwa kuwa Gazeti la Tanzania Daima halitaruhusiwa kuchapishwa wala kusambazwa popote nchini au nje ya nchi, klufuatia uamuzi wa kusitisha leseni ya gazeti hilo. Uamuzi huu unatokana na kukithiri na kujirudia kwa makosa yanayokiuka sheria za nchi,” amesema Kipangula

“Juhudi za kuwaonya, kuwaelekeza na kuwakumbusha wahariri wa gazeti hilo,  kufuata masharti ya leseni kwa muda wa mwaka mmoja sasa, zimeshindwa kuzaa matudna kutokana na ukaidi.”

Hata hivyo, Kipangula amesema, Tanzania Daima linaweza kukata rufaa juu ya uamuzi huo, kwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, ndani ya siku 30.

Au, kuomba upya leseni kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari, ili kuruhusiwa kurejea kuchapisha na kusambaza.

“Wanayofursa ya kuomba tena leseni kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari ili kuruhusiwa kurejea kuchapisha na kusambaza, watakapoona wamejitafakari na kuwa tayari kufuata taratibu. Vile vile wanayo nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 30 kama hawajaridhika na uamuzi huu,” amesema Kipangula.

Aidha, Kipangula amevikumbusha vyombo vingine vya habari kutii sheria na kufuata misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.

“Serikali inavipongeza vyombo vingine vinavyoendelea kutii sheria na kufuata misingi ya taaluma na haitasita kuchukua hatua kali wakati wowote kwa watakaokiuka taratibu za kisheria na misingi ya taaluma muhimu ya habari,” amesema Kipangula

error: Content is protected !!