HATIMAYE Serikali ya Tanzania kwa mara ya kwanza imetoa kauli kuhusu Mtanzania, Nemes Tarimo aliyefariki dunia vitani nchini Ukraine akiipigania Urusi na kusisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania hakuna Mtanzania anayeruhusiwa kujiunga na jeshi la nchi nyingine.
Nemes ambaye pia alikuwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alijiunga na kikundi Cha kijeshi cha Urusi kinachofahamika kama Wagner kwa makubaliano ya kuachwa huru kutoka katika kifungo cha miaka saba gerezani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo tarehe 24 Januari, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax amesema mwili wa Tarimo unatarajiwa kuwasili nchini muda wowote baada ya kuanza kuondoa Urusi leo asubuhi.
Aidha, ameongeza kuwa mbali na Tarimo kuahidiwa kuachiwa huru, pia aliahidi kupewa kiasi cha fedha pindi mapigano yakiisha.
Dk. Tax amesema Tarimo aliyekwenda masomoni nchini Urusi 2020, alifariki dunia mwishoni mwa Oktoba mwaka jana.
Amesema alijiunga na kikundi cha Wagner baada ya Machi 2022 kuhukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani kwa makosa ya kufanya vitendo vya uhalifu.

“Tumepokea taarifa kutoka Serikali ya Urusi kuwa akiwa gerezani Tarimo alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi Cha kijeshi cha Urusi – Wagner kwa ahadi ya kupewa fedha na kuachwa huru mara baada ya vita kumalizika, alikubali kujiunga na alipelekwa Ukraine kwa ajili ya mapigano tarehe 24 Oktoba 2022.
“Serikali imeshirikiana na Serikali ya Urusi kuhakikisha mwili huo unawasili nchini, ambapo umesafirishwa asubuhi ya leo hivyo wakati wowote utawasili Tanzania,” amesema.
Dk. Tax amewataka watanzania kutii sheria za nchi wakiwa ndani na nje ya nchi, huku akikumbusha kwamba ni kinyume cha sheria na katiba kwa Mtanzania kujiunga na jeshi la nchi nyingine.
“Nikumbushe kwa mujibu wa sheria za nchi Mtanzania yeyote hatakiwi kujiunga na jeshi la nchi nyingine, kitendo hicho ni kuvunja Sheria za nchi yako, unatakiwa kujiunga na jeshi la nchi yetu kwa taratibu zilizopo. Katiba iko wazi wazi Mtanzania haturuhusiwi kujiunga na jeshi lingine,” amesema Dk. Tax.
Dk. Tax amesema Tarimo alikwenda nchini Urusi na kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA), mwaka 2020 kwa masomo ya Shahada ya Uzamili katika fani ya Business Informatics.
Leave a comment