May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yafungua milango utafiti wa DNA kwa makabila Tanzania

Spread the love

 

SERIKALI imesema ipo tayari kushirikiana na watafiti kufanya utafiti wa vinasaba kwa makabila mbalimbali nchini ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu ya magonjwa kwa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea). 

Hatua hiyo imekuja baada ya Chama cha Watafiti wa Vinasaba nchini kuanza mchakato wa kufanya utafiti wa vinasaba kwa makabila mbalimbali nchini.

Akifunga kongamo la 13 la watafiti wa vinasaba Afrika leo tarehe 2 Septemba 2021 jijini Dar kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na watoto- Zanzibar, Nassor Mazrui amesema utafiti huo ni muhimu kwa zama za sasa

Mazrui amesema watu wengi wanadhani kuwa vinasaba hutumika kuainisha uhalisia wa mzazi wa mtoto pekee jambo ambalo si kweli.

“Elimu hii ya vinasaba ni muhimu sana kwa sababu tunaweza kutumia utafiti huu wa vinasaba kupata tiba ya magonjwa mbalimbali ambayo ni adimu.

“Hata sasa tumeathiriwa na Corona kwa zaidi ya miaka miwili, hivyo mchango wa watafiti hawa unaweza kuibua mapya katika matibabu ya magonjwa ya aina hii ndio maana nasema sisi Zanzibar na serikali ya Jamhuri kwa ujumla tunafungua milango kwa watalaam wetu,” amesema.

Aidha, Mwenyekiti wa Chama hicho cha watafiti wa vinasaba Tanzania, Siana Nkya amesema utafiti huo wa vinasaba utakaoanza hivi karibuni utasaidia watalaam wa afya kung’amua mambo mengine kwani kuna utofauti mkubwa wa vinasaba kati ya kabila na kabila.

“Mpangilio wa vinasaba ni tofauti kwa sababu unaamua hiki tunachokiona nje ya mwili wa binadamu. Ndio maana baba na mama wakizaa watoto wawili, wanatofautiana muonekana,” amesema.

Amesema baadhi ya magonjwa yanaweza kuepukwa mathalani selimundu kwa kupima vinasaba.

“Waafrika walishirikishwa katika utafiti wa vinasaba kwa mara ya kwanza mwaka 1990, tena ilikuwa asilimia mbili tu ya utafiti mzima, hivyo sasa tunahitaji kufanya utafiti mkubwa hasa ikizingatiwa Waafrika ndio chimbuko la binadamu kama historia inavyosema,” amesema.

Mwakilishi wa chama cha magonjwa adimu, Togolani Mavura amesema vinasaba vina nguvu katika kutibu magonjwa adimu.

Amesema asilimia 70 ya magonjwa adimu kwa watoto duniani yameshindikana kutibika, hivyo muamko wa tafiti hizo utasaidia upatikanaji wa matibabu hayo kwa urahisi.

error: Content is protected !!