Tuesday , 27 February 2024
Home Habari Mchanganyiko Serikali yaenda kufanya upekuzi mwingine kwa Kabendera
Habari Mchanganyiko

Serikali yaenda kufanya upekuzi mwingine kwa Kabendera

Spread the love

ERICK Matugwa Kabendera, mwandishi wa habari za kichunguzi, mtafiti, na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, uchumi na usalama wa kikanda, bado anaendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama nchini Tanzania, kwa siku tano mfululizo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa tulizozipata muda huu kutoka ndani ya jeshi la Polisi zinasema, maofisa wa jeshi hilo, kwa sasa wanaelekea nyumbani kwake, Mbweni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya upekuzi mpya.

Haijaweza kufahamika mara moja, upekuzi huo unalenga nini. Tayari Kabendera amepukuliwa na maofisa uhamiaji na kuchukua hati yake ya kusafiria.

“Yawezekana kinachotafutwa sasa, ni komputa yake mpakato. Ni kawaida ya polisi kuchukua komputa hizo kwa watu wanaowatuhumu kwenye makossa hayo,” ameeleza Saed Kubenea, mwandishi wa habari za uchunguzi na mbunge wa Ubungo.

Kabendera anashikiliwa katika kituo cha Polisi Kati (Centro), jijini Dar es Salaam. Anatuhumiwa kuchapisha habari za uwongo kwenye mitandao ya kijamii, kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.

Anatuhumiwa kuandika habari hiyo yenye kichwa cha maneno, “Another critic of President John Magufuli is silenced” – Mkosoaji mwingine wa Rais Magufuli anyamazishwa – kwenye gazeti la The Economist.

Mbali na kufanya kazi za uandishi wa habari, Kabendera amekuwa akifanya kazi za ushauri wa masuala mbalimbali ya kiuchumi na kisiasa na Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na baadhi ya balozi zilizopo nchini.

Kabla ya jeshi la Polisi kudai kuwa Kabendera anashikiliwa kwa tuhuma za kuandika, kuchapisha na kusambaza taarifa inazosema ni za “uwongo,” Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alinukuliwa akisema, jeshi lake linamshikilia mwandishi huyo wa kujitegemea, “kutokana na utata wa uraia wake.” 

Mambosasa aliwaambia waandishi wa habari Jumanne iliyopita, tarehe 29 Julai kuwa tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu, Kabendera amekamatwa kutokana na “kukaidi amri ya jeshi la Polisi.”

Alisema, jeshi hilo lilikuwa linataka kumhoji kuhusu utata wa uraia wake, lakini yeye aligoma kuitikia wito huo, jambo ambalo alidai liliwalazimisha Polisi kuvamia nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa ndugu, watu waliofika nyumbani kwa Kabendera kumkamata walikuwa sita na walijitambulisha, lakini waligoma kutoa vitambulisho vyao.

Waliomkamata Kabendera walieleza wanafamilia kuwa wanampeleka mwandishi huyo wa habari katika kituo cha polisi Oysterbay.

Hata hivyo, hatua ya Polisi kudai kuwa limemkamata na kumshikilia Kabendera kutokana na madai ya uraia wake, kuliibua mjadala mpana miongoni mwa makundi ya waandishi wa habari, ikiwamo sababu ya Polisi kujiingiza kwenye kutaka kufahamu suala la uraia wa mwandishi huyo, wakati kazi hiyo hufanywa na Idara ya Uhamiaji.

Sakata la uraia wa Kabendera, liliibuka kwa mara ya kwanza mwaka 2013, lakini baadaye mamlaka nchini humo zilithibitisha kuwa mkosoaji huyo mkubwa wa sera za chama kilichoko madarakani, ni raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Erick Matuga Kabendera, ni mtoto aliyezaliwa na Nolasco John Kabendera na Periviana Kokumanyika Protase. Wazazi wake wote wawili – Nolasco (Baba) na Periviana (Mama) – wamezaliwa Tanzania. Naye Erick, ni mzaliwa Bukoba, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Erick Kabendera, ni mtoto wa tisa kwa baba yake Nolasco na wanne kwa mama yake Periviana.

Kabla ya jeshi la Polisi kumshikilia kwa siku tatu na bila kumpa dhamana, Kabendera alikuwa anashikiliwa na maofisa wa idara ya uhamiaji, kwa makossa ambayo tayari yalishajadiliwa na kufungwa mwaka 2013.

Kwa mujibu wa sheria ya uraia ya Tanzania ya mwaka 1995, hakuna mwanya wowote unaoweza kumfanya Kabendera kutiliwa mashaka uraia wake, ameeleza wakili mmoja wa mahakama kuu, ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

Anasema, “hii ni kwa sababu, Erick amezaliwa Tanzania. Wazazi wake wawili, wamezaliwa Tanzania. Hivyo kama labda wazazi wa wazazi wake (babu) yake hakuwa Mtanzania, basi wanaopaswa kuulizwa, ni wazazi wa Erick na siyo yeye.

“Kwa maneno mengine, huwezi kuhoji urai wa Erick, kabla hujahoji uraia wa wazazi wake.”

Mbali na taarifa kwenye gazeti la Economist ambazo zinadaiwa na Polisi kuwa mwandishi huyo anatuhimiwa kutenda makossa ya mtandaoni – Cybecrime Act – kifungu cha 16,   wiki iliyopita, Kabendera aliandika makala kwenye gazeti la The East Africa, inayokosoa uamuzi wa Rais Magufuli, kumuondoa Janury Makamba, kutoka kwenye baraza lake la mawaziri.

Kabendera, ni mmoja wa marafiki wa karibu wa January na kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa kutumia ukaribu wake huo, alisaidia kampeni na mikakati ya CCM, kushinda uchaguzi huo.

Shirika la waandishi wa habari barani Afrika (CPJ), limeeleza masikitiko yake kufuatia ya hatua ya serikali ya kumkamata Kabendera na imezitaka mamlaka za Serikali ya Tanzania kumwanchia mara moja.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mafua yamtesa Papa, afuta mikutano

Spread the loveKiongozi wa Kanisa katoliki duniani, Papa Francis amelazimika kufuta mkutano...

Habari Mchanganyiko

Oryx wagawa mitungi 1000 kwa viongozi wa dini, wajasiriamali Moshi

Spread the loveVIONGOZI wa dini kutoka madhehebu mbalimbali pamoja na wajasiriamali katika...

Habari Mchanganyiko

RC Geita awafunda wahitimu wapya GGML

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ametoa wito kwa...

Habari Mchanganyiko

Biteko asisitiza umuhimu wa EREA sekta ya nishati

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!