Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali yaelemewa na mzigo wa wafanyakazi hewa, yanusurika kupigwa Sh. 11.1 bil
Habari za SiasaTangulizi

Serikali yaelemewa na mzigo wa wafanyakazi hewa, yanusurika kupigwa Sh. 11.1 bil

Dk. Philip Mpango
Spread the love

SAKATA la watumishi hewa, sasa limeingiza serikali kwenye mzigo mkubwa wa malimbikizo ya mishahara, MwanaHALISI Online linaripoti.

Taarifa kutoka wizara ya fedha na mipango (WFM), ofisi ya rais, menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora na Tamisemi zinasema, serikali inakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni uliotokana na hatua yake ya kusitisha malipo ya mishahara kipindi cha uhakiki wa watumishi hewa.

Hata hivyo, uhakiki wa wafanyakazi hewa, pamoja na kuingiza serikali katika tatizo la malimbikizo ya mishahara na madai mengine, lakini linaelezwa kuwa limeokoa mabilioni ya shilingi za umma, kutokana na kuwapo kwa baadhi ya madai feki.

Kwa mujibu wa mawasiliano kati ya katibu mkuu wa wizara ya fedha na yule wa TAMISEMI, hadi kufikia tarehe 1 Julai 2017, madai ya malimbikizo ya mishahara kwenye mfumo yalifikia Sh. 127. 6 bilioni. Malipo haya ni kwa watumishi 82,111.

“Madai hayo, ni kwa watumishi wa umma ambao bado utumishi wao haujakoma,” taarifa ya katibu mkuu wizara ya fedha inaeleza.

Anasema, “madai haya yameongezeka kutoka Sh. 8,444,445,356 mwezi Juni 2016 sawa na ongezeko la Sh. 119,160,683,516.81 kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.”

Katibu mkuu huyo wa wizara ya fedha anasisitiza, “ongezeko hili limesababishwa na serikali kusitisha malipo haya kupisha zoezi la kuwabaini watumishi hewa ndani ya utumishi wa umma.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizara ya fedha ilipokea ankara za madai za watumishi yakiwemo malimbikizo ya mishahara iliyopitishwa na kuhakikiwa na ofisi ya rais, menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora.

Baada ya zoezi hilo la uhakiki wa watumishi kukamilika, serikali inasema, “tumeanza kujipanga kuanza kulipa madai haya kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara (LAWSON).

Haikuweza kufahamika mara moja, serikali ni lini itakamilisha mchakato wake huo wa kulipa malimbikizo ya wafanyakazi wake.

Taarifa hiyo inasema, “katika kufanikisha kazi hii, wizara ya fedha na mipango kupitia idara yake ya bajeti iliandaa hadidu za rejea na kuunda timu kwa ajili ya kufanya uhakiki kwa watumishi wa wizara, idara na taasisi za serikali, ofisi za sekretarieti za mikoa na halmashauri wenye madai yanayozidi Sh. 40 milioni.

“Kazi hii ilifanyika na kukamilika kwa muda wa wiki mbili kuanzia tarehe 23 Oktoba 2017 hadi tarehe 4 Novemba 2017.”

Kwa mujibu wa katibu mkuu wizara ya fedha, uhakiki wa wafanyakazi hewa umeonyesha kuwa madai ya watumishi 76 kati ya 110 yenye jumla ya Sh. 4,102,260,190.02 sawa na asilimia 26.9 ya madai yote yameonekana kuwa ni halali.

Madai ya watumishi 34 yenye jumla ya Sh. 11,167,601,688.98, yameonekana siyo halali kwa sababu yamekosa vigezo vya uhalali wake.

Kiasi hiki ni sawa na asilimia 73.1 ya madai yote ya shilingi 15,269,861,879.81 ambayo yangelipwa kwa watu wasiostahili endapo kusingefanyika uhakiki.

Kuhusu mafanikio ya kufanyika uhakiki, taarifa inasema, zoezi hilo la uhakiki wa sehemu ya madai ya malimbikizo ya mishahara limeweza kuokoa jumla ya Sh. 11.167 bilioni sawa na asilimia 73.1 ya fedha ambazo zingepotea endapo malipo haya yangefanyika bila kufanya uhakiki.

Kwa kuwa uhakiki wa madai ya watumishi 110 umebaini kasoro nyingi timu inashauri kuwa ufanyike uhakiki wa madai yote yaliyobakia ya watumishi 82,001 yenye jumla ya shilingi 123,345,949,807.32 yaliyopo kwenye mfumo kabla ya kulipwa ili madai halali tu ndio yalipwe.

Baadhi ya changamoto zilizyojitokeza katika zoezi hili ni pamoja na kutopatikana kwa baadhi ya vielelezo na nyaraka za madai katika majalada ya watumishi.

Matatizo mengine yaliyopatikana, ni ucheleweshaji wa kuidhinishwa watumishi kwenye vyeo vya madaraka wanavyokaimu na uwepo wa maafisa wenye vyeo vidogo (mfano TGSD) kukaimu vyeo vya madaraka makubwa (LSSE) ambao husababisha madai ya malimbikizo ya mshahara kuwa makubwa.

Serikali inatumia zaidi ya Sh. 5 bilioni kulipa mishahara na stahiki nyingine za wafanyakazi wake wa umma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!