Serikali imesema ipo mbioni kukamilisha taratibu za kuutangaza zabuni ya kufufua kiwanda cha kutengeneza matairi cha General tyre kilichopo mkoani Arusha ifikapo Oktoba, 2023 ili kumpata mwekezaji mahiri mwenye mtaji na teknolojia ya kisasa inayohitajika. Anaripoti Isaya Temu, TUDARCo…(endelea).
Hayo yamesemwa leo tarehe 30 Agosti 2023 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilombero, Abubakari Asenga (CCM), aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kufufua kiwanda hicho cha General Tyre.
Akijibu swali hilo, Kigahe ameeleza kuwa Serikali ipo kwenye mpango wa kufufua kiwanda hicho kwa kutafuta mwekezaji mwenye uwezo unaohitajika na wizara hiyo.
Amesema mradi wa kiwanda hicho mchakato upo kwenye hatua ya kukamilisha taratibu za kuutangaza zabuni ifikapo mwezi Oktoba, 2023 ili kumpata mwekezaji mahiri mwenye mtaji na teknolojia ya kisasa inayohitajika.
Amesema zabuni ya mradi huo inatarajiwa kutangazwa ndani na nje ya nchi.
Aidha, katika swali la nyongeza, Assenga aliihojia Serikali ina mpango gani wa kufufua shamba la mpira lililopo kata ya Mwaya-Kilombero.
Akijibu swali hilo, Naibu waziri huyo amesema; “Kwa upande wa mashamba ya mpira likiwemo shamba la Kilombero, Serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) imeendelea kuboresha uzalishaji wa mpira kwa kupanda miche mipya, kujenga miundombinu, kununua mashine za kugemea utomvu, uchakataji na vitendea kazi vingine ili kuongeza upatikanaji wa utomvu na mpira mkavu wenye viwango bora.”
Leave a comment