Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali yaanika hali ya uchumi nchini
Habari za SiasaTangulizi

Serikali yaanika hali ya uchumi nchini

Dk. Philip Mpango
Spread the love

PAMOJA na watanzania wengi kuendelea kulalamika kwa madai kuwa wana hali mbaya ya kiuchumi serikali imesema kuwa uchumi wa taifa huko imara na ukikua kwa asilima 7.1 ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita. Anaripoti Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mbali na kuwa uchumi unaendelea kukua, serikali imeeleza kwamba washirika wa maendeleo wamekuwa wakisuasua kutoa fedha kwa wakati kama wanavyokuwa wameahidi.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Fedha Mipango, Dk. Philipo Mpango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa na Utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha miezi sita katika bajeti ya 2018/19.

Dk Mpango alisema kuwa Washirika wa Maendeleo wameendelea kusaidia bajeti ya Serikali kupitia miradi na programu mbalimbali.

Alisema kuwa kwa mwaka 2017/18, Washirika wa Maendeleo waliahidi kuchangia Bajeti ya Serikali kiasi cha Sh. 3.97 trilioni hadi kufikia Juni 2018, hata hivyo alieleza kuwa Washirika wa maendeleo walitoa kiasi cha Sh. 2.46 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 62 ya ahadi.

Aidha alisema kuwa Katika mwaka 2018/19, Washirika wa Maendeleo waliahidi kuchangia bajeti ya Serikali kiasi cha Sh. 2.67 trilioni hadi kufikia Novemba, 2018, na kiasi kilichopokelewa ni Sh. 498.5 bilioni, sawa na asilimia 54 na kiasi cha Sh. 928.7 bilioni kilichotarajiwa kupatinaka katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2018.

Dk.Mipango alisema kuwa Kasi ndogo ya utoaji fedha inatokana na Masharti magumu ya wafadhili na majadiliano kuchukua muda mrefu.

Aidha alieleza kuwa kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi katika sekta na hivyo kusababisha fedha za awamu zinazofuata kuchelewa kutolewa.

Pato la Taifa.

Akizungumzia pato la taifa Dk. Mpango alisema kuwa pato la taifa kwa bei za mwaka 2007 Uchumi wa Taifa umeendelea kuwa imara, ukikua kwa asilimia 7.1 (2017) ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa asilimia 7.0 kwa miaka miwili iliyopita (2015-2016).

Alifafanua kuwa Kwa nchi za EAC, uchumi wa Tanzania ulikua kwa kasi zaidi (7.1%) mwaka 2017 ukilinganisha na Rwanda (6.1%), Uganda (5.1%), Kenya (4.9%), na Burundi (0.0%), Vilevile, Tanzania iliongoza katika ukuaji wa uchumi kwenye nchi za SADC.

Alisema kwamba katika kipindi cha Januari hadi Juni 2018, Pato la Taifa lilikua kwa 7.0% ikilinganishwa na 6.3% katika kipindi kama hicho mwaka 2017 na kubainisha Sekta zilizokua kwa kasi zaidi kuwa ni sekta ya ujenzi (15.7%), Uzalishaji viwandani (12.0%), habari na mawasiliano (11.2), na uchukuzi na uhifadhi mizigo (8.2%).

“ Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi 5 bora kwa kasi ya ukuaji wa uchumi katika bara la Afrika katika nusu ya kwanza ya 2018, ikijumuisha nchi ya Ethiopia (8.5%), Ivory Coast (7.4%), Rwanda (7.2), Tanzania (7.0%), na Senegal (7.0%).

“Sekta zilizoendelea kutoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa (Januari – Juni 2018) ni Kilimo (34.5%), Ujenzi (16.8%) na Biashara (10.1%). Aidha, sekta ya kilimo ilikua kwa 3.6% kwa kipindi hicho. Napenda kwa niaba ya Serikali kuwapongeza wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya ujenzi kwa mchango wao mkubwa katika uchumi wa Taifa” alisema Waziri.

Kwa upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dk. Mpango aliwaonya wafanyakazi wa TRA kuachana na tabia ya kutumia lugha mbaya ya kuwakarahisha walipakodi na kuwafungia maduka wafanyabiashara na badala yake watumie nafasi yao kuwaelimisha wafanyabiashara hao.

“Napenda kuwasisitiza tena watumishi wote wa TRA kutoza kodi kwa mujibu wa sheria za kodi na kanuni zake. Kama maandiko matakatifu yanavyoelekeza: “Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa” (Luka 3:11-16).

“Makadirio ya kodi yasiwe kandamizi. Aidha, ninaukumbusha uongozi wa TRA utekeleze maagizo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha TRA kilichofanyika Mwalimu Nyerere Convention Centre tarehe 10 Disemba 2018.

“Utaratibu wa kumfungia mfanyabiashara biashara yake ili kushinikiza alipe kodi anayodaiwa, sasa usitishwe isipokuwa kwa mkwepa kodi sugu na kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa TRA! Badala yake, TRA ijikite zaidi kutoa elimu kwa mlipa kodi juu ya utunzaji wa vitabu vya hesabu za biashara, na kumpa fursa ya kufanya naye majadiliano kuhusu mpangilio bora wa kulipa malimbikizo ya kodi kwa mkupuo au kwa awamu pamoja na adhabu stahiki kama zilivyobainishwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Kodi 2015.

“Matumizi ya lugha mbaya, vitisho na ubabe dhidi ya walipa kodi wenye historia nzuri ya kulipa kodi stahiki yasipewe nafasi kabisa, na pale inapothibitika kwenda kinyume na maadili mema basi mtumishi husika awajibishwe mara moja kwa kuzingatia taratibu za kiutumishi. Vilevile, mtumishi wa TRA yeyote anayetuhumiwa kupokea au kudai rushwa asimamishwe kazi mara moja kupisha uchunguzi wa vyombo husika (TAKUKURU na Jeshi la Polisi).

“Aidha ninaiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuongeza jitihada za kudhibiti biashara ya magendo inayoendeshwa na wafanyabiashara wanaopitisha mizigo bandari bubu kwa nia ya kukwepa kodi hususan eneo la mwambao wa bahari ya Hindi na sehemu zote za mipakani na kuhakikisha kodi stahiki inalipwa mara moja na bidhaa zilizokamatwa kutaifishwa,” alisema Dk. Mpango.

Mfumuko wa Bei

Kuhusu Mfumuko wa bei alisema kuwa umeendelea kupungua kutoka wastani wa aslimia 4.3 mwaka 2017/18 hadi kufikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea katika miaka ya karibuni cha asilimia 3.0 mwezi Novemba 2018.

“Kati ya Julai hadi Novemba 2018, Tanzania ilikuwa na kiwango kidogo zaidi cha mfumuko wa bei ikilinganishwa na nchi ya Uganda asilimia 3.3 na Kenya asilimia 4.8

sababu zilizochangia mfumuko wa bei kuwa chini ni pamoja na Upatikanaji mzuri wa chakula katika masoko ya ndani na nchi jirani, ambapo uzalishaji wa chakula nchini ulifikia tani million 15.9 ikilinganishwa na mahitaji ya tani million 13.3 kwa kipindi hicho, hivyo kuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 120, Mfumuko wa bei ya chakula ulifikia asilimia 2.0 Novemba 2018 ikilinganishwa na asilimia 7.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2017 Kutengamaa kwa bei za mafuta katika soko la dunia na Utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na za bajeti” alisema Dk Mpango.

Hali ya maisha ya mwananchi

“Kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi imepelekea kuimarika kwa hali ya maisha ya wananchi hasa wale waliopata fursa za ajira (na kipato) katika shughuli za kiuchumi zinazokua haraka, kama vile ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, reli, upanuzi wa bandari na viwanja vya ndege, mauzo ya mazao ya kilimo, ujenzi wa viwanda na utoaji wa huduma za fedha na mawasiliano. Kuongezeka kwa ujenzi wa nyumba bora za kuishi, umiliki wa mali zisizohamishika na vyombo vya usafiri, na vifaa vya kudumu vya majumbani (consumer durables) vinaashiria kuimarika kwa hali ya maisha ya wananchi.

“Aidha, ukuaji mzuri wa uchumi umeiwezesha Serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato na kugharamia uboreshaji wa huduma za jamii hususan elimu (ikwemo elimu-msingi bila ada), afya (hospitali, vituo vya afya, zahanati, madawa, vifaa-tiba, vitendanishi), maji na kuimarisha uzalishaji wa umeme na kuusambaza vijijini.

“Kutokana na kiwango kidogo cha mfumuko wa bei, uwezo wa shilingi kununua vitu ni mkubwa (Nguvu ya buku 10 acha kabisa!). Aidha, gharama za maisha kwa mwananchi kwa ujumla, zimeongezeka kwa kasi ndogo” alieleza Waziri.

Thamani ya Shilingi

Akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari alisema kuwa Thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa tulivu, alieleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Novemba 2018, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,276, ikilinganishwa na shilingi 2,235 katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2017.

“ Hivyo, shilingi ilipungua thamani dhidi ya dola (depreciation) kwa asilimia 1.8, kiwango ambacho ni kidogo na hakikuathiri utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania ikizingatiwa kuwa mfumuko wa bei wa wastani katika nchi washirika wakuu wa biashara na Tanzania ni asilimia 3.0.

“Utulivu wa thamani ya shilingi umetokana na utekelezaji wa sera ya fedha, usimamizi thabiti wa mapato na matumizi ya Serikali, kutumia gesi asilia katika kuzalisha umeme, na baadhi ya viwanda kuzalisha bidhaa ambazo awali zilikuwa zikiagizwa kwa wingi kutoka nje, mfano, vigae” alieleza.

Utekelezaji wa Sera ya Fedha

Alisema kuwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2018/19, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilichukua hatua mbalimbali kuongeza ukwasi kwenye uchumi ili kuziwezesha benki za biashara kuongeza utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Miongoni mwa hatua.

Alizitaja baadhi ya hatua kuwa ni Kutoa mikopo ya muda mfupi kwa mabenki Kushusha riba ya mikopo kwa mabenki kutoka asilima 9.0 hadi asilimia 7.0 Agosti 2018 na Kununua fedha za kigeni kutoka katika benki za biashara na taasisi za Serikali.

Hatua nyingine ni Kutokana na hatua hizo, ukwasi kwenye mabenki ya biashara uliongezeka na riba katika masoko ya fedha zilipungua, Riba ya siku moja katika soko la fedha baina ya mabenki ilishuka kutoka asilimia 3.72 Oktoba 2017 hadi wastani wa asilimia 2.29 Oktoba 2018.

Alizitaja hatua nyingine kuwa ni Riba za dhamana za Serikali zilipungua kutoka 9.41% hadi kufikia wastani wa asilimia 7.40 Oktoba 2017,Riba za mikopo inayotolewa na mabenki ilipungua kwa kiasi kidogo kutoka wastani wa asilimia 18.1 kati ya Julai na Oktoba 2017 hadi asilimia 17.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.

Akiba ya Fedha za Kigeni

“Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kutosheleza mahitaji ya kuiwezesha Tanzania kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje na pia kujenga imani ya wawekezaji.

“Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani 5,079.0 milioni mwezi Novemba 2018, kiasi ambacho kinatosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi 5.

“Kiwango hiki cha akiba ya fedha za kigeni ni zaidi ya lengo la Serikali kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayokidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4. Pia ni zaidi ya lengo la miezi 4.5 lililowekwa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki” alisema Dk. Mpango.

Mwenendo wa Sekta ya Kibenki

“Sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara, salama na yenye kutengeneza faida, ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha zaidi ya kiwango kinachotakiwa kisheria.

“Uwiano wa mitaji ya mabenki ikilinganishwa na rasilimali zao ulikuwa 16.3%, ikiwa juu ya kiwango kinachohitajika kisheria cha asilimia 10.0.

“Kiwango cha mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu ikilinganishwa na kiwango cha amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi kilifikia 36% ikilinganishwa na kiwango cha chini kinachohitajika kisheria cha asilimia 20.

“Hii inaashiria kuwa mabenki yana ukwasi wa kutosha kwa ajili ya shughuli zake za kila siku ikiwemo kulipa madeni pamoja na kutoa mikopo,Katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2018, sekta ya kibenki ilipata faida ya Sh. 285.4 bilioni (ikilinganishwa na Sh. 317.0 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2017). Kupungua kwa faida kulitokana na kuongezeka kwa tengo la hasara kufuatia kuanza kutumika kwa Kanuni za Kimataifa za Utoaji Taarifa za Fedha (International Financial Reporting Standard 9 – IFRS9) mwezi Januari 2018.

“Mikopo chechefu iliendelea kushuka hadi kufikia asilimia 9.7 ya mikopo yote Septemba 2018 kutoka 12.5% iliyorekodiwa mwishoni mwa Disemba 2017.

“ Kuendelea kupungua kwa mikopo chechefu kulitokana na hatua zilizochukuliwa na BoT ikiwa pamoja na Kuzitaka benki zote kutekeleza mikakati ya kuboresha utoaji na usimamizi wa mikopo, ikiwemo uchambuzi wa maombi ya mikopo, na kutumia kwa lazima taarifa ya historia za wakopaji kabla ya kutoa mkopo na Benki zote kutakiwa kuazisha idara maalum kwa ajili ya kufuatilia ukusanyaji wa madeni chechefu.

“Sekta ya kibenki pia imeendelea kukua hadi Septemba 2018, kulikuwa na jumla ya Benki na Taasisi za fedha zinazosimamiwa na BOT zipatazo 61. Kati ya hizo, mabenki yalikuwa 52 yenye matawi 884 nchini kote na zingine zilikuwa taasisi zinazotoa huduma za kifedha,” alisema.

1. Mwenendo wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali

Mapato ya Serikali

Dk. Mpango alisema kuwa katka kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya mwaka 2018/19 (Julai – Novemba), makusanyo ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yalifikia Sh. 7.37 trilioni sawa na asilimia 88.9 ya makadirio ya Sh. 8.30 trilioni katika kipindi hicho.

Aidha alisema kuwa Mapato ya kodi yalifikia Sh. 6.23 trilioni ikiwa ni asilimia 88 ya lengo la kukusanya Sh. 7.04 trilioni kwa kipindi hicho, aidha alisema kuwa Mapato yasiyo ya kodi yalifikia Sh. 936.03 bilioni sawa na asilimia 21 zaidi ya lengo la Sh. 775.36 bilioni huku akisema mapato ya Mapato ya Halmashauri yalifikia Sh. 203.8 bilioni sawa na asilimia 61 ya lengo.

“Ongezeko la mapato yasiyo ya kodi limetokana na kuimarishwa kwa ufuatiliaji kwenye Taasisi, Mashirika na Kampuni kulikoiwezesha Serikali kupata michango na gawio stahiki kutoka kwenye uwekezaji wake, Kuimarika kwa matumizi ya Technolojia katika ukusanyaji wa maduhuli kwenye Wizara na Idara zinazojitegemea kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato uitwao Government Electronic Payment Gateway (GePG) ambapo kati ya Julai 2017 hadi Novemba 2018, jumla ya Taasisi za Serikali 325 zinatumia mfumo huu kukusanya maduhuli.

“Jitihada za kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara: Serikali kupitia Sheria ya Fedha 2018/19 Serikali ilipunguza ada na tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa wananchi. Miongoni mwa ada na tozo zilizopunguzwa ni pamoja na tozo za mazingira, OSHA, FIRE, TBS, TFDA na tozo kwenye madini ya chumvi.

“Changamoto za ukusanyaji wa mapato ni pamoja na ukwepaji wa kodi; mwamko mdogo wa wananchi kudai risiti pale wanapofanya manunuzi na wafanyabiashara kutoa risiti pale wanapofanya mauzo na wigo mdogo wa kodi,” alieleza.

Deni la Serikali

Waziri alisema kuwa kufikia Septemba, 2018 deni la Serikali lilifikia Sh. 49.37 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 3.2 ikilinganishwa na Sh. 47.82 trilioni Septemba 2017 Deni la ndani lilikuwa Sh. 13.64 trilioni sawa na asilimia 27.6 na deni la nje ni Sh. 35.72 trilioni sawa na asilimia 72.4.

“Nchi kuwa na deni sio dhambi, jambo muhimu ni kuhakikisha kuwa fedha tulizokopa zinatumika kujenga rasilimali ambazo ni msingi wa kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mali na kulipa mikopo hiyo,” alisema.

Uhimilivu wa Deni

Waziri alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo Dhamana na Misaada Sura 134, Serikali inawajibu wa kufanya tathmini ya uhimilivu wa deni (DSA) kila mwaka ili kupima mwenendo wa deni na uhimilivu wake.

“Matokeo ya awali ya tathmini iliyofanywa Desemba 2018 inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Matokeo haya yanafanana na tathmini iliyofanywa na IMF. Deni la umma limeendelea kuwa himilivu,” alisema .

Matarajio Hadi Juni 2019

Alisema kuwa Uchumi unatarajiwa kuendelea kukua kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kwenye miundombinu wezeshi ya uzalishaji mali kama vile barabara, madaraja, bomba la mafuta, ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa na viwanja vya ndege; Ujenzi wa kituo cha kufua umeme utokanao na nguvu za maji katika mto Rufiji chenye uwezo wa kuzalisha 2,100MW kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani; na Maboresho katika sekta ya madini na kilimo; na uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi (EPZ/SEZ).

“Tunatarajia pia kuwa viwanda vilivyojengwa na vitakavyojengwa vitachangia zaidi Pato la Taifa kwa kuchochea uzalishaji mali hasa bidhaa za kilimo na kuongeza thamani ya bidhaa. Aidha, mapato ya ndani yanatarajiwa kuongezeka kutokana na hatua mbalimbali za Serikali kukuza uchumi na kupanua wigo wa mapato.

“Pia, maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji yanayoendelea kutekelezwa na Serikali yanatarajiwa kushawishi na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi.

“Mfumuko wa bei unatarajia kuendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja isiyozidi asilimia 5.0 katika kipindi cha muda wa kati. Thamani ya shilingi ya Tanzania inatarajiwa pia kubaki kuwa imara.

“Nakisi ya urari wa biashara ya nje inatarajiwa kupungua kufuatia mikakati ya kuongeza thamani na mauzo ya mazao ya kilimo na madini kwa kutumia viwanda vya ndani, na kuimarika kwa shughuli za utalii na huduma za usafirishaji kwenda nchi jirani.

“Akiba ya fedha za kigeni itaendelea kuwa ya kuridhisha na kutosheleza mahitaji ya fedha za kigeni na kwa kiwango cha kutosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.5 kilichowekwa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alieleza.

Changamoto Katika Nusu ya Pili ya 2018/19

Dk Mpango alisema kwamba pamoja na na kukua kwa uchumi na matarajio ya kuimarika kwa ukuaji, zipo changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuathiri mwenendo wa Uchumi wa Taifa na utekelezaji wa bajeti ya 2018/19 ambazo ni Kuongezeka kwa gharama za mikopo kwenye masoko ya fedha duniani kutokana na mabadiliko ya sera za fedha katika nchi kubwa kiuchumi (hususan Marekani na nchi za Ulaya) na kupungua kwa misaada ya kibajeti na fedha za washirika wa maendeleo za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali inaongeza nguvu kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupanua wigo na vilevile kuimarisha usimamizi wa matumizi ya Serikali.

Aidha alieleza kuwa Serikali inatafuta vyanzo vingine vya mikopo ya nje vyenye masharti nafuu katika nchi za Mashariki ya Kati na Mashariki ya mbali.

“Mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuathiri uzalishaji hususan katika sekta mama ya kilimo ambapo sehemu kubwa bado tunategemea mvua. Mkakati wa Serikali ni kuongeza nguvu kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, kuhifadhi vyanzo vya maji, kuhimiza matumizi ya mbegu bora za mazao ikiwa pamoja na yanayohimili ukame, na kuongeza jitihada za kutafuta masoko ya uhakika ya mazao.

“Mvutano wa kiuchumi baina ya Marekani na China unaopelekea nchi hizo kuwekeana kodi za kulipizana kisasi (retaliatory tariffs) unaweza kuathiri biashara kati ya Tanzania na China kutokana na uwezekano wa kuongezeka kwa bei ya bidhaa tunazoagiza kutoka China. Ili kujihami, Serikali imejielekeza kupanua wigo wa bidhaa na huduma tunazouza nje (hasa utalii) na nchi washirika wa biashara.

“Uwezekano wa kupanda kwa bei za mafuta kwenye soko la dunia kutokana na Marekani kuiwekea tena vikwazo nchi ya Iran na vita vinavyoendelea Syria, na Yemen. Mkakati wa Serikali kukabiliana na changamoto hiyo ni kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na gesi asilia na vyanzo vingine mbadala, pamoja na ujenzi wa bwawa na mtambo wa kufua umeme Mto Rufiji,” aliweka Bayana Dk. Mpango.

Hata Dk. Mpango hivyo alisema kuwa anawaalika wadau wote wa kodi na wananchi kwa ujumla kutuletea kwa maandishi mapendekezo na ushauri kuhusu vyanzo vipya vya mapato ya Serikali na marekebisho ya viwango vya kodi kwa ajili ya bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2019/20 na ninaomba mapendekezo hayo yawasilishwe kwa maandishi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango kabla ya tarehe 10 Februari 2019.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!