September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yaahidi kuwalinda wafanyakazi

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imeahidi kupambana na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu katika maeneo ya kazi, anaandika Regina Mkonde.

Hayo yamesemwa na Alfred Mapunda, Kaimu Mkurugenzi wa Sera katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wakati akizindua ripoti ya haki za binadamu na biashara kwa mwaka 2015 iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), jijini Dar es Salaam.

Mapunda alikuwa akizungumza baada ya kuzindua ripoti hiyo kwa niaba ya Dk. Adelhelm Meru, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, ambapo amesema serikali itandelea kufanyia kazi tafiti zinazofanywa na LHRC ili kuhakikisha inaondoa changamoto zinazowakabili wananchi.

“Sekta ya viwanda ndiyo kipaumbele chetu na mkakati wa serikali ni kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinazingatia katika maeneo yote ya kazi,” amesema huku akieleza zaidi kuwa;

“Tunashukuru LHRC kwa kuja na mpango huu na kuhakikisha ripoti hii inapatikana katika kipindi kwa miaka minne mfululizo.”

Helen Kijo Bisimba, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC amesema kuwa ripoti hiyo inaonesha matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayofanyika katika meneo ya kazi.

“Katika kampuni tulizofanyia utafiti huu tumebaini kuwa asilimia 63.8 ya wafanyakazi waliohojiwa walikuwa wanafanya kazi bila ya mikataba hata wenye mikataba, asilimia 90 wanafanyakazi tofauti na tulizoona katika mikataba yao,” amesema Kijo Bisimba.

Amesisitiza kuwa lengo la LHRC ni kuisaidia serikali katika kuhakikisha kampuni, mashirika na taasisi zote hapa nchini zinatoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wake.

“Serikali ikifanikiwa katika hili, itapata mapato lakini pia wafanyakazi nao watapata manufaa na kufurahia sheria za ajira kulingana na sheria ya ajira ya mwaka 2014,” amesema.

Hii ni ripoti ya nne mfululizo kutolewa na LHRC tangu mwaka 2012 ambapo utafiti wa mwaka jana ulihusisha mikoa 16 ambayo ni sawa na asilimia 53 ya mikoa yote hapa nchini huku wafanyakazi 722 na kampuni 55 zikishirikishwa.

error: Content is protected !!