Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali ya Tanzania yasalimu amri kwa wafadhili
Habari za SiasaTangulizi

Serikali ya Tanzania yasalimu amri kwa wafadhili

Dk. Philip Mpango
Spread the love

SERIKALI ya Tanzania inajiandaa kuwasilisha bungeni, muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Takwimu, ili “kuondoa kibano” cha kunyimwa fedha za maendeleo kutoka kwa nchi wahisani.” Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Taarifa kutoka ndani ya serikali na mashirika ya fedha ya kimataifa – Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) – zinasema, serikali imelazimika kurekebisha sheria hiyo, kufuatia WB na IMF kuzuia mabilioni ya dola za Kimarekani kwa Tanzania.

Benki ya dunia imetenga takribani dola za Kimarekani 1.7 bilioni (karibu Sh. 4.1 trilioni), kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Lakini sehemu kubwa ya fedha hizo, zimezuiliwa baada ya kupitishwa kwa sheria mpya ya Takwimu.

Mashirika ya fedha ya kimataifa, wakiwamo benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa, wameungana na wadau wengine nchini, kudai kuwa sheria mpya ya Takwimu inakiuka haki za binadamu na kuminya uhuru wa wananchi wa kujieleza na ule wa kutoa maoni.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, serikali imepanga kuwasilisha bungeni marekebisho ya vifungu kadhaa vinavyolalamikiwa ili “kujinusuru na kibano hicho.”

Muswaada wa mabadiliko ya sheria hiyo, unatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti unaoendelea mjini Dodoma. 

Taarifa zinasema, muswada huo, utakuja bungeni kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza, mwezi Juni mwaka huu.

Bunge la Jamhuri, lilipitisha mabadiliko ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2018, katika mkutano wake wa Septemba mwaka jana. Mabadiliko hayo yalipata upinzani mkali kutoka kwa makundi ya wanaharakati na wabunge wa upinzani. 

Hata hivyo, muswada huo ulipitishwa kwa mbwembwe bungeni, baada ya serikali kutumia wingi na wabunge wake wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Pamoja na mambo mengine, sheria mpya ya Takwimu inapiga marufuku uchakataji wa taarifa za tawimu na imeweka marufuku ya kusambaza taarifa zote za takwimu bila ruhusa ya serikali.

Aidha, sheria inaelekeza kuwa kila anayetoa taarifa za takwimu kuthibitishwa kwanza na serikali. Sheria inatamtaka kuwa ni kosa la jinai kuchakata na kusambaza taarifa za takwimu bila ruhusa ya serikali. Sheria inatoa hadi adhabu ya kifungo kwa atakayekiuka masharti hayo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka jijini Dar es Salaam na makao makuu ya benki ya dunia nchini Marekani zinasema, benki imekasirishwa na hatua ya serikali kupitisha sheria hiyo na imeshinikiza kuondolewa kwa baadhi ya vifungu kandamizi, haraka iwezekanavyo.

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI ONLINE ambaye ni mmoja wa maofisa wa ngazi ya juu wa IMF amesema, benki ya dunia imesisitiza, “haitarejesha hata dola moja ya fedha zake za maendeleo, kabla ya serikali kurekebisha sheria hiyo.”

Amesema, uamuzi wa benki hiyo, umetokana na “kujiridhisha kuwa sheria mpya ya Takwimu, “inaminya uhuru wa wananchi wa kupata taarifa na kinyume na unapingana na Katiba ya Jamhuri na mikataba ya kimataifa.” 

Vifungu ambavyo vipo kwenye Sheria ya Takwimu (2018) na ambavyo serikali imeahidi wahisani kuvifanyia marekebisho, ni pamoja na kifungu cha 24 (A) (2); 24 (B) (1) pamoja na 24 (B) (2). 

Serikali imekubali kukiondoa pia kifungu kinachotoa adhabu kwa watu wanaopatikana na hatia ya kukiuka sheria hiyo.

Mtoa taarifa huyo anasema, kuwasilishwa kwa mabadiliko ya sheria ya Takwimu katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti, ni sehemu ya makubaliano kati ya ujumbe wa serikali na maofisa wa ngazi ya juu wa benki ya dunia na IMF. 

Mazungumzo kati ya pande hizo mbili, yaliyofanyika wiki mbili zilizopita, jijini Washington DC, nchini Marekani.

Anasema, katika mkutano huo, taarifa zinasema, ujumbe wa Tanzania uliweza kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa WB anayeshughulikia masuala ya Afrika, Hafez Ghanem na Mkurugenzi Mtendaji wa benki anayesimamia nchi za Afrika, Anne Kabagambe.

Fedha ambazo zimeondolewa na WB kutokana na kuwapo kwa sheria hiyo, ni pamoja na dola za Marekani 450 milioni, zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya kusaidia miradi ya TASAF 111 na dola za Kimarekani 300 milioni, zilizokuwa zitolewe kwa ajili ya mradi wa maji safi vijijini na maji taka.

Mamilioni mengine yaliyozuiwa, ni dola za Marekani 400 milioni, zilizokuwa zimeombwa kwa ajili ya kuongeza ubora wa elimu ya sekondari.

Anasema, pamoja na kuwapo kwa sheria ya Takwimu, wahisani wamekasirishwa pia na hatua ya serikali ya kuweka zuio  kwa wasichana waliopata mimba wakiwa shule za Sekondari kuendelea na mfumo rasmi wa elimu.

“Kule Marekani wakuwa hawa waliwaambia wazi wazi, maofisa wa Tanzania kuwa upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo inayo gharamiwa kwa mikopo nafuu ya Benki ya Dunia, haitatolewa iwapo serikali haitarekebisha kasoro hizo,” ameeleza afisa huyo wa WB.

Anasema, “serikali imekubali kufanyia marekebisho kasoro hizo, ikiwa ni pamoja na kuahidi kuwawezesha wasichana waliopata mimba shule za Sekondari kuendelea na masomo.”

Tangu kufanyika kwa mabadiliko kwenye sheria ya takwimu, watu kadhaa, wakiwamo wabunge na taasisi za kitafiti za ndani, zimeshindwa kuchambua na kuchapisha taarifa tofauti na zile za serikali hasa katika suala tata la ukuaji wa uchumi wa taifa.

Wakati serikali ikidai kuwa uchumi wake umezidi kuimarika, baadhi ya wabunge hasa wa upinzani, wamekuwa wakiituhumu serikali ya Rais John Pombe Magufuli, kudanganya kwenye taarifa zake za ukuaji wa uchumi.

Baadhi ya wakosoaji wa serikali kuhusu taarifa zake za ukuaji wa uchumi (GDP Growth Rate), wanadai kuwa wameshindwa kutoa taarifa mbadala kwa kuogopa mkono wa sheria, unaotokana na kuwapo kwa sheria hiyo.

Mpaka sasa, angalau Zitto Kabwe, mbunge kutoka chama cha ACT- Wazalendo, kutokea jimbo la Kigoma Mjini, mkoani Kigoma, Magharibi mwa Tanzania, ndiye anayeonekana kutumia kinga ya Bunge, kukosoa serikali kuhusu taarifa zake za ukuaji wa uchumi.

Zitto amekuwa akisema bungeni, kuwa uchumi wa nchi umedorora; kuna tofauti kubwa ya kipato kati ya matajiri na maskini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RUWASA yachongewa, yateketeza mamilioni kwa maji yenye magadi

Spread the loveSAKATA la ukosefu wa maji wilayani Momba mkoani Songwe limezidi...

error: Content is protected !!