SERIKALI ya Tanzania, inatarajia kununua tani 735,000 za chakula, zinazotosheleza kwa matumizi ya nchi nzima, katika kipindi cha mwezi mmoja. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Akizungumza bungeni jijini Dodoma, leo tarehe 12 Mei 2020, Japhet Hasunga, Waziri wa Kilimo, amesema mpango huo ni tahadhari ya nchi, dhidi ya athari za ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosabishwa na Virusi vya Corona (Covid-19).
Hasunga amesema mahitaji ya nafaka kwa mwezi kwa Watanzania wote ni tani 750,000, na kwamba kwa sasa NFRA haina kiasi hicho cha akiba.
Amesema kwa sasa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) utakuwa na tani 103,698, baada ya tani 65,000 zenye thamani ya Sh. 39 bilioni, kununuliwa .
“Wizara kupitia NFRA itanunua tani 65,000 kutokana na fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya 2019/2020 Sh. 15 bilioni na mapato ya ndani Sh. 24 bilioni, ili kuifanya hifadhi ta chakula kuongezeeka kufikia tani 103,698.794 ambayo inajumlisha akiba ya tani 38,698.794,” amesema Hasunga
“Tukichukulia asimilia 20 ya Watanzania ndiyo pekee watakaohitaji kununua chakula kwa asilimia 100, ambao mahitaji yao ya nafaka kwa mwezi yatakuwa tani 145,000. Kiasi hicho cha chakula ni kidogo endapo dharura ya mahitaji ya chakula yatatokea.”
Kufuatia changamoto hiyo, Hasunga amesema Serikali ina mpango wa kupata tani 735,000, ambapo wizara yake itazungumza na wizara ya fedha na mipango, ili kuwezesha NFRA, kupata fedha Sh. 217 bilioni kwa ajili ya kununua tani 435,000 .
Hasunga amesema tani 300,000 zilizobaki, zitanunuliwa na NFRA kupitia bajeti iliyotengwa katika mwaka 2020/2021 pamoja na mapato ya wakala huo. Hivyo kufanya jumla ya chakula kitakachonunuliwa kuwa tani 735,000.
Wakati huo huo, Hasunga amesema wizara yake kwa kushirikiana na sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa zilizoko pembezoni mwa mipaka ya nchi, itaendelea kudhibiti utoroshwaji wa chakula nje ya nchi, kupitia njia za panya.
“Wizara itaimarisha usafirishaji wa chakula kutoka kwenye mikoa yenye upungufu,” amesisitiza Hasunga.
Leave a comment