August 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali ya Tanzania kujenga gereza kila Wilaya 

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imesema, ina mpango wa kujenga magereza kila wilaya, ili kumaliza tatizo la mrundikano wa mahabusu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mpango huo umeelezwa leo Alhamisi tarehe 11 Juni 2020 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani wakati akijibu swali la Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge Viti Maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kisangi  alihoji mkakati wa serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo, ili kuwalida wafungwa na mahabusu na magonjwa ya milipuko.

Katika maswali yake, Kisangi amesema Gereza l a Segerea jijini Dar es Salaam lina mrundikano mkubwa wa wafungwa, ambapo alihoji Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hilo hilo.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, amesema Serikali ina mpango wa muda mrefu wa kujenga magereza hayo kwa awamu, kadri hali ya bajeti itakavyoruhusu.

“Serikali ina mpango wa muda mrefu ambao ni kujenga magereza kila Wilaya zisizokuwa na magereza kwa awamu ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam kadri ya hali ya bajeti itakavyoruhusu,” amesema Waziri huyo.

Waziri huyo amekiri uwepo wa changamoto hiyo, akisema kwamba imetokana na ukuaji wa uchumi katika jiji la Dar es Salaam, uliosababisha ongezeko la vitendo vya uhalifu.

Amesema ongezeko la uhalifu limepelekea Gereza la Mahabusu Segerea kukabiliwa na changamoto ya msongamano wa mahabusu.

“Kutokana na kasi ya ukuaji wa uchumi katika Mkoa wa Dar es Salaam, hali hiyo imesababisha ongezeko la uhalifuna kupelekea Gereza la Mahabusu Segerea kukabiliwa na changamoto ya msongamano wa mahabusu,” amesema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, amesema kwa sasa Serikali inakabiliana na changamoto hiyo kwa kuwahamisha mahabusu kwenye magereza yenye nafasi, pamoja na kufanya mawasiliano na taasisi za uchunguzi na uendeshaji kesi, ili mashauri yao yapatiwe ufumbuzi na kumalizika kwa wakati.

“Kufuatia changamoto hiyo, Serikali kupitia Jeshi la Magereza imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto hiyo, mathalani kuwahamisha baadhi ya mahabusu kwenye magereza yenye nafasi, “ amejibu Waziri huyo na kuongeza:

“Kuendelea kufanya mawasiliano na taasisi mbalimbali za kiuchunguzi na kimaamuzi zenye kuhusika na uendeshaji wa kesi za mahabusu ili mashauri yao yaweze kupatiwa ufumbuzi na kumalizika kwa wakati,” amesema.

error: Content is protected !!