April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali ya Tanzania: Hatujasema hatuna corona

Dk. Hassan Abbas, katibu mkuu wizara ya habari

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imeeleza, haijawahi kusema haina maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19). Anaripoti Regina Mkonde …(endelea).

“Hatujawahi kusema, hatuna virusi vya corona. Tanzania ni sehemu ya dunia, kwa hiyo tunao raia wa kigeni wanaokuja nchini kwa shughuli mbalimbali.”

“Tunao raia wetu wanaokwenda nje ya nchi na kama tunavyojua, dunia imepata hilo tatizo, hivyo muingiliano upo,” ameeleza Dk. Hassan Abbasi, Msemaji Mkuu wa Serikali.

Dk. Abbas ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), tarehe 11 Februari 2021 kuhsu mlipuko wa COVID-19 nchini Tanzania.

Amesema, pamoja na ugonjwa huo kuwepo nchini, serikali ilikuwa makini na kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana nao kwa kutumia njia za kisayansi na asili.

“Kwa hiyo serikali ilikuwa makini tangu mapema, lakini hatuwezi kusema Tanzania haina na haijawahi kuwa na mgonjwa wa Covid-19, hatuwezi kusema hivyo,” amesema.

Alipoulizwa sababu za serikali kusitisha kutoa takwimu za mwenendo wa Covid-19, Dk. Abass amedai, wamesitisha kutoa takwimu kwa sababu, wamefanikiwa kudhibiti maambukizi.

“Hatuwezi focus (jikita) sana au kuwekeza kwenye kusema tuna wagonjwa wangapi sababu kwa kiasi kikubwa sana tumedhibiti,” ameeleza.

Gervas Nyaisonga, Rais wa baraza la Maskofu

Amesema, kuna raia wa kigeni wanaoingia Tanzania na baada ya kufanyiwa vipimo wamegundulika kuwa na corona; na au raia wa Tanzania wanaokwenda nje na kurejea nchini kisha kungudulika kuwa na virusi hivyo, imekuja wakati huu, ambako zimekuwapo taarifa nyingi kuhusu watu kupoteza ndugu na jamaa zao.

Miongoni mwa waliofariki dunia na kuleta wasiwasi, ni pamoja na familia ya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo mkoani Morogoro (SUA), Prof. Delphina Mamiro.

Prof. Delphina na familia yake ya watu wanne – baba na mama – wamefariki dunia ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Prof. Delphina alianza kujisikia vibaya mwanzoni mwa mwezi huu na kufariki dunia wakati alipokuwa akipatiwa matibabu; siku chache baadaye mumewe akafariki dunia.

Wazazi wake, Prof. Delphina walifariki dunia tarehe 13 na 16 Januari 2021, mkoani Kilimanjaro.

Aidha, kauli ya Dk. Abass imekuja wakati kuna nyaraka na barua za kichungaji, zilizotolewa na baadhi ya madhebu ya kidini na jamii ya wasomi, wakitaka wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na virusi vya Corona.

Katika waraka wake wa Jumatatu iliyopita – tarehe 8 Februari – kwa wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Eliphas Bisanda, ametaka kuwapo uangalifu wa kujilinda na maambukizi ya virusi vya Corona ikiwa ni pamoja na kuepuka misongamano na kuvaa barakoa.

Hata hivyo, waraka wa Prof. Bisanda, “umebatilishwa” na wizara ya Sayansi na tekronolijia kwa maelezo kuwa “haukufauta taratibu za wizara ya afya.”

Katika waraka wa Kanisa la Katoliki ulitolewa na Rais wa Baraza la Maaskofu (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga, kanisa limetaka waaumini wake na wananchi kwa ujumla, kuchukua hatua zote kujikinga na Corona.

Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo, ameeleza katika barua yake ya kichungaji, umuhimu wa watu kuendelea kujikinga.

Askofu Frederick Shoo, Mkuu wa Kanisa la KKKT

Barua ya Askofu Dk. Shoo iliyotumwa kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT, maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wa Kanisa ilisema, “Corona bado ipo” na hivyo basi, “ni muhimu watu wakaendelea kujikinga.”

Kwa mara ya mwisho Tanzania kutoa takwimu za wagonjwa wa Covid 19 ilikuwa Aprili mwaka jana. Kisa cha kwanza kuripotiwa cha kuwapo kwa mgonjwa wa Covid-19, kilikuwa Machi 2020.

Katika taarifa yake ya 29 Aprili 2020, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa alisema, takribani watu 480 waliambukizwa ugonjwa huo, huku 16 wakiwa wamefariki dunia.

Waziri Majaliwa alitoa taarifa hiyo siku tano baada ya aliyekuwa Waziri wa Afya wakati huo, Ummy Mwalimu – 24 Aprili – kutoa takwimu za mwenendo wa ugonjwa huo.

Tanzania ilisitisha zoezi hilo kwa maelezo ya kufanya maboresho kwenye maabara ya taifa, kufuatia kubainika dosari katika baadhi ya maeneo, ikiwemo moja ya mashine ya kupimia na mfumo wa kuhifadhia vipimo.

Baadae zoezi la upimaji Covid-19, lilihamishiwa katika maabara ya Mabibo, jijini Dar es Salaam, ambayo imeelezwa kuwa ni maabara ya kisasa.

error: Content is protected !!