July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CHADEMA: Serikali ya JK inavunja sheria ya kura ya maoni

Spread the love

SERIKALI itakuwa inatenda kosa la jinai kujiingiza katika kushawishi wananchi kuiridhia katiba inayopendekezwa ambayo imepitishwa na Bunge Maalum la Katiba.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013, kazi ya kutangaza katiba inayopendekezwa kwa nia ya kuelimisha wananchi itaratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na siyo chombo kingine chochote.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu alisema kitendo chochote kitakachofanywa na Ikulu au ofisi nyingine yoyote ya serikali, kinacholenga kushawishi wananchi wairidhie katiba, ni kuvunja sheria.

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema Ikulu itakuwa imejiingiza katika uvunjaji wa sheria za nchi kutekeleza mkakati wa kuhamasisha Watanzania kuikubali na kuipigia kura ya NDIO katiba inayopendekezwa.

“Kitendo cha serikali ya Rais Kikwete, mawaziri wake na maofisa wa serikali yake kutaka kutumia fedha za umma kufanya kampeni kwa katiba inayopendekezwa na CCM kwa Watanzania sio tu ni matumizi mabaya ya fedha za umma bali pia ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi hii,” alisema Lissu.

Amesema Lissu kwamba Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Salva Rweyemamu kusema, “Kila kitu kinakwenda kwa sheria, hata hizo fedha zitatolewa na serikali kama ambavyo ilitoa za kugharamia Bunge Maalum” hakutoshi kuhalalisha uvunjaji wa sheria. Kwenyewe ni kinyume cha sheria.

Amesema maadili na sheria za uchaguzi zikiwemo Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013, Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 zitahusika na masuala yoyote yanayohusu matumizi ya fedha wakati wa kura ya maoni.

“Sheria zetu za uchaguzi na maadili zinakataza kitendo kinachofanywa na Ikulu. Ni kosa la jinai kwa mijibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya 2010, sehemu ya tano ya hii sheria inazungumzia vitendo vinavyokatazwa,” alisema Lissu.

Lissu amesema sheria hiyo inataja mwenendo usiostahili kuwa ni: Wakati wa mchakato wa uchaguzi, kampeni za uchaguzi au uchaguzi, kitendo kinachokatazwa ni kile mtu ambaye kabla au kipindi cha kampeni, moja kwa moja au kwa namna nyingine yoyote kupitia kwa mtu mwingine yeyote.

Au kwa niaba yake anatoa, anakopesha au anakubali kutoa au kukopesha au anatoa, anaahidi au kumpatia au anajaribu kumpatia fedha yeyote au kitu kingine chochote chenye thamani mpiga kura.

“Au mtu yeyote kwa niaba ya mpiga kura yeyote au mtu mwingine yeyote kwa nia ya kumshawishi mpiga kura kupiga kura au kuacha kupiga kura au kumrubuni mtu yoyote kuacha kutenda kitendo hicho katika kura za maoni na uchaguzi, sheria imekataza,” amesema Lissu.

Akifafanua kuhusu kifungu cha cha 21 (1) (a) cha sheria ya gharama za uchaguzi kuwa malipo yasiyofaa: Kila mtu ambaye kwa njia ya rushwa yeye mwenyewe au kumtumia mtu mwingine yeyote kwa niaba yake ama kabla

Wakati wa uchaguzi kwa uwazi au kwa kificho anatoa au anaandaa au analipa kwa ujumla au kwa sehemu gharama ya kuandaa kinywaji au chakula au mahitaji ya mtu yeyote kwa nia ya kumshawishi mtu huyo au mtu mwingine yeyote kupiga kura sheria inakataza.

“Hivyo Rais ameonesha kwa mwenendo au kwa maneno ya Salva kwamba anataka kushiriki mchakato wa kupata katiba, hivyo wanakatazwa pia na kifungu cha 25 cha sheria ya gharama za uchaguzi, hawawezi kuhalalishwa haya makosa yanatendwa na Rais hayawezi kuwa halali.

“Matendo ya kihunikihuni ya namna hii yatawafanya watu waingie barabarani na kuchoma moto mabunge, kama ilivyotokea Burkina Faso wiki iliyopita. Uhuniuhuni wa namna hii, dharau kwa wananchi za namna hii ndizo zinazovunja amani,” alisema Lissu.

Lissu alisema ni vizuri Tume ya Taifa ya Uchaguzi izungumze hadharani kama wanachokifanya Ikulu na chama cha CCM ni halali.

Alisema Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unakusudia kupeleka malalamiko NEC kuhusu mpango huo wa Serikali ya Rais Kikwete kutaka kutumia fedha za umma kutekeleza mpango wa kushawishi wananchi waikubali katiba inayopendekezwa kwa kupiga kura ya NDIO.

error: Content is protected !!