January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali watangaza kiama kwa waajiri

Spread the love

SERIKALI  imetangaza kiama kwa waajiri wote nchini ambao watakuwa kikwazo katika uanzishwaji wa vyama vya wafanyakazi katika sehemu za kazi. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mbali na kutangaza kiama, waajiri wametakiwa kuhakikisha wanatoa fursa kwa vyama vya wafanyakazi  kuanzishwa kwenye maeneo yao ya kazi ili viweze kupunguza migogoro baina ya wafanyakazi na waajiri.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu wa bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama wakati akizungumza na wanachama wa chama cha wafanyakazi nchini wa viwandani, biashara, taasisi za fedha, huduma na ushauri (Tuico) kwenye mkutano mkuu wa tano wa chama hicho mjini Dodoma.

Mhagama amesema kuwa kuna baadhi ya waajiri nchini ambao wamekuwa miungu watu na hawataki wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi nchini kitendo alichosema ni ukiukwaji wa sheria za nchi.

“Kuna baadhi ya waajiri ambao ni majipu sugu, wanajua kabisa sheria inawataka wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi nchini lakini hawataki kufanya hivyo, niwaagize waajiri wote nchini kutoa fursa katika maeneo yao ya kazi kuanzishwa kwa vyama vya wafanyakazi ili kupitia vyama hivyo migogoro yao iweze kutatuliwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Mhagama na kuongeza:

“Kwa mwajiri yeyote ambaye atazuia wafanyakazi wake kujiunga na vyama vya wafanyakazi nchini atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.”

Aidha alimwagiza Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicolaus Mgaya kufuatilia utendaji kazi wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi mahali pa kazi na endapo utendaji wao wa kazi utakuwa hauridhishi waondolewe baada ya utaratibu wa kisheria kufuatwa.

Amesema hiyo inatokana na baadhi yao kuwa vyanzo vya migogoro baina ya wafanyakazi na waajiri kutokana na viongozi hao kuacha kutekeleza majukumu yao ya kuwatetea wafanyakazi na badala yake wanaungana na waajiri kuwakandamiza wafanyakazi wenzao.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi kutetea maslahi ya wafanyakazi kwani pamoja na majukumu mengine waliyonayo ni jukumu lao la msingi kutetea maslahi ya wafanyakazi wanaowatumikia.

error: Content is protected !!