CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kuwa uhaba wa mbolea nchini umesababishwa na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh. 325 bililioni, kwa makampuni yaliyopewa kazi ya kuagiza na kuuza mbolea ya ruzuku nchini. Anaripoti Kenneth Ngelesi, kutoka Mbeya …. (endelea).
Hayo yameelezwa leo na aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Mbozi, Paschal Haonga, katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo alifafanua kuwa tatizo la uhaba wa mbolea hasa za kukuzia, linasababishwa na serikali kushindwa kutekelezwa wajibu wake.
Haonga ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Bunge na Wananchi, amesema kuwa shida siyo mbolea kutoroshwa nje, bali ni serikali kudaiwa na waingizaji wa bidhaa hiyo.
Alisema, “tumewasikia viongozi wa serikali, akiwemo waziri mkuu, Kassim Majaliwa na waziri wa kilimo, Hussein Bashe, kwamba eti uhaba wa mbolea, unatokana na utoroshwaji wa mbolea nje ya nchi. Hili si kweli.”
Aliongeza, “uhaba wa mbolea, unatokana na deni linalodaiwa serikali kwa wasambazaji wa mbolea. Serikali ilipe deni hili kama kweli imedhamiria kuwasaidia wakulima na kuacha kubabaisha.”
Kwa mujibu wa Haonga, bajeti ya mbolea ya ruzuku kwa mwaka wa fedha 2022/2023, ni Sh. 150 bilioni, lakini mpaka sasa serikali inadaiwa Sh. 350 bilioni, na kwamba sababu ya deni hilo, ni kutokuwapo taarifa sahihi za mahitaji kwa nchi nzima.

Alisema, uhaba wa mbolea unatokana na wafanyabishara kuhofia kudhulumiwa na serikali kama ambavyo ilivyotokea mwaka 2014, ambapo pamoja na serikali kuingia makubaliano ya kusambaza mbolea za ruzuku kwa wakulima, lakini waligoma au kuchelewa kulipa malipo waliyotakiwa.
“Mwaka 2014, tukiwa bungeni, mambo haya yalijitokeza. Serikali ilijifunga mkataba na wafanyabiashara kuleta mbolea, lakini baadaye wakagoma kuwaliwa kwa kujificha kwenye kichaka cha uhakiki wa madeni na kuna taarifa mpaka wengi wao, hawajalipwa madai hayo,” alieleza.
Alisema, matokeo yake, makampuni mengi yanayoagiza mbolea pamoja na mawakala yamesitisha kufanya hivyo, kutokana na hofu ya kuingizwa mjini.
Alidai kuwa baadhi ya wafanyabiashara aliozungumza nao, wamemueleza kuwa wameamua kuweka mgomo wa chini kwa chini wa usambazaji wa mbolea ya ruzuku, kutokana na madai kuwa hadi Januari 15 mwaka huu serikali inadaiwa Sh. 325 bilioni.
Haonga ameendelea kudai kuwa wafanyabishara wanaogopa kuingia kwenye biashara ya ruzuku licha kwa mbolea kuwepo, lakini pia wanashangaa kuona serikali inatoa sababu kuwa uchache wa mbolea unachangiwa na utoroshwaji, huku wakiacha ukweli kwamba tatizo linatokana na deni.

Kutokana na kadhia hiyo, Chadema wanaitaka serikali ichukue hatua za dharura kulipa madeni kwa makampuni yaliyoagiza mbolea kwa kuwa wengi wao mtaji yao wamekopa kutoka taasisi za kifedha, na kwamba ucheleweshwaji wa malipo utawatesa wakulima.
“Kama ilivyo utamaduni wa Chadema, tunaibua hoja lakini pia tunatoa na njia za kutatua. Katika hili la mbolea, serikali ilipe madeni haya na kama ina dhamira ya kuendelea kuuzwa mbolea kwa njia ya ruzuzu, basi iboreshwe mifumo yake na kuziondoa changamoto zilizopo,” alifafanua.
Alisema, katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Songwe Rukwa, Iringa na Tabora, mbolea ambayo ilipaswa kuuzwa kwa Sh. 70, 000 (elfu sabini), inauzwa Sh. 100,000 (laki moja), na hivyo kuondoa kabisa dhana ya kuwapo mbolea ya ruzuku.
Katika hatua nyingine, Haonga alisema, changamoto nyingine, katika sakata la Mbolea ni ukiritimba.
Alisema, kitendo cha Serikali kuwaagiza makampuni kuuza mbolea moja kwa moja nalo likawa kuangalia kwani linachangia kuleta ukiritimba katika zoezi zima la usambazi wa mbolea ya ruzuku.
Leave a comment