August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali wagoma kuifuta kodi ya umiliki wa vyombo vya moto

Askari wa Usalama barabarani akikagua kibali cha kodi ya umiliki wa gari

Spread the love

SERIKALI imesema ada ya mwaka ya Magari (Annual Motor Vehicle Lincese Ownership Fees) inatozwa kwa wamiliki wa vyombo vya moto kwa mujibu wa Sheria ya Usalama barabarani ya mwaka 1973 ambapo mmiliki wa chombo cha moto hutakiwa kulipa ada  ya kila mwaka, anaandika Dany Tibason.

Hayo yalielezwa leo bungeni na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni (CCM).

Chegeni aliuliza kuwa serikali haioni umuhimu wa kurekebisha Road Licence au ifutwe ili ukusanyaji wa kodi hiyo uendane na matumizi halisi ya vyombo vya moto vya barabara.

Akijibu swali hilo, Dk. Kijaji amesema ada ya mwaka ya magari inatozwa kwa wamiliki wa vyombo vya moto kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 (Road Trafick Art 1973).

Amesema  mmiliki wa chombo cha moto hutakiwa kulipa ada ya kila mwaka kwa kuanzia tarehe ya mwezi wa kwanza ambapo chombo kilisajiliwa.

Dk. Kijaji amesema ada hiyo inatozwa kulingana na ukubwa wa ingini ya chombo husika huku msingi wa tozo hiyo ni umiliki wa chombo (Motor Vehicle Ownership Linence) na siyo matuzimi ya chombo barabarani (Road Licence).

‘’Hivyo basi mmiliki wa chombo hutakiwa kulipa ada hiyo bila kujali kama chombo kimetumika katika mwaka husika au hakijatumika,’’ amesema Dk Kijaji.

Naibu Waziri huyo amesema ada ya mwaka ya umiliki wa chombo cha moto inaweza kusitishwa kulipwa endapo mmiliki wa chombo cha moto atatoa taarifa kwa kamishna wa kodi na kudhibitishwa kuwa chombo hicho cha moto hakitumiki tena kutokana na sababu mbalimbali kama ajali.

Aisha amesema serikali imepokea mapendekezo na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Chegeni wakitaka ada ifutwe au ilipwe kulingana na matumizi ya chombo cha moto.

‘’Napenda kuliarifu bunge lako tukufu  kuwa serikali itafanya mapitio ya sheria na kanuni ya umiliki na matumizi  ya vyombo vya moto ili kupata njia bora ya kukusanya kodi hiyo kwa sasa itaendelea kulipwa kwa utaratibu uliopo.

error: Content is protected !!