August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali, wafanyabiashara mifugo wavurugana

Spread the love

UMOJA wa Wafanyabishara wa Mifugo na Mazao yake Kinondoni (Uwaminaki), umelalamikia utaratibu mpya wa serikali wa kutoza kodi ya Sh. 18,500 kwa kila ng’ombe, anaandika Faki Sosi.

Gharama hiyo inajumuisha bidhaa hiyo baada ya kununuliwa kwenye soko la Mkoa wa Pwani na kupelekwa katika machinjio ya Kimara Suka, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchinjwa.

Ramadhan Dule, Mwenyekiti wa Uwaminaki amesema, ni wiki ya pili sasa machinjio ya Kimara Suka yamefungwa na serikali baada ya wafanyabiashara hao kupinga kulipa kodi.

Amesema, jambo lingine wanalopinga ni kitendo cha kuwalazimisha wafanyabiashara hao kupitisha mifugo yao katika mnada wa Pungu kufanyiwa uchunguzi wa afya wakidai ni usumbufu na kuwaongezea gharama.

“Tunanunua ng’ombe Mkoa wa Pwani na kulipia ushuru wa 6,500 halafu eti tunatakiwa kuwafikisha soko la Pugu kupimwa na hapo tutatakiwa kulipa tena ushuru wa 6500, tukifika Soko la Kimara Suka tulipe ushuru wa 5,500 hivi kweli nyama itauzwa kwa shilingi ngapi ili faida ipatikane,”amehoji Dule.

Suala hilo lilikuwa na mvutano kwa muda mrefu hali iliyosababisha kufikia hatua ya kwenda mahakamani kupinga ushuru huo na kuamuliwa kwamba, wakati kesi ikiendelea wafanyabiashara waendelee kufanya biashara kwa utaratibu wa kulipa Pwani na Soko la Kimara pekee.

“Cha kushangaza uongozi wa Kimara umefungia machinjio hayo kwa madai kuwa, ni agizo kutoka wizarani bila ya kutaja hasa muhusika aliyetoa agizo,” amesema Dule.

Amesema kuwa, kutokana na kufungwa machinjio hiyo kumesababisha baadhi ya ng’omba kufa kwa kukosa chakula kutokana na kukaa kwa muda mrefu.

Akizungumzia hatua ya kupelekwa mifugo hiyo Pugu, amesema ni usumbufu na unyanyasaji wa viumbe ikiwemo kuwasababishia wafanyabiashara kutumia gharama kubwa.

Diwani wa Kata ya Saranga, Ephraim Kinyafu asema kuwa ameshangazwa na hatua ya baadhi ya watendaji wa Manispaa ya Kinondoni kukaa kimya wakati wakiendelea kuzuia machinjio hiyo ambako kunaikosesha mapato.

“Hapa kuna vijana zaidi ya 400 wamejipatia ajira, kwa kitendo cha kufunga machinjio hiyo wana hatari ya kukosa ajira zao,” amesema Kinyafu.

error: Content is protected !!