December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali, wadau wakutana kujadili hatua za mwisho maboresho sheria ya habari

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imekutana na wadau wa sekta ya habari, kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yameelezwa leo tarehe 21 Novemba 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

“Tuna kikao na wadau wa habari kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,” amesema Nape.

Kikao hicho kinafanyika ikiwa zimepita siku kadhaa, tangu Nape aeleze kuwa Serikali ilishindwa kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya sheria hiyo, ili kutoa nafasi kwa wadau kupitia kwa mara ya mwisho marekebisho hayo kwa ajili ya kukwepa mivutano baada ya sheria kupitishwa.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa habari kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Ambapo wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.

Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebishon dhidi ya kifungu chake cha 7 (2)(b)(lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na Serikali, wakidai kinaingilia uhuru wa uhariri.

error: Content is protected !!