May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali: Mhandisi Mfugale alifariki ghafla

Spread the love

 

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi nchini Tanzania, imesema aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale (67), alifariki ghafla. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mhandisi Mfugale alifikwa na mauti saa 5:00 asubuhi, tarehe 29 Juni 2021, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma.

Leo Ijumaa, tarehe 2 Julai 2021, Mwili wa Mhandisi Mfugale, unaagwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, ambapo viongozi mbalimbali wamehudhuliwa akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Malongo amesema, Mhandisi Mfugale alizaliwa tarehe 1 Desemba 1953, Kijiji cha Ifunda mkoani Iringa.

Watoto wa Mhandisi Patrick Mfugale

Amesema, enzi za uhai wake, marehemu amefanya kazi wizara ya ujenzi kuanzia mwaka 1975 na kwa nafasi ya mkurugenzi mkuu ni kuanzia mwaka 2011 hadi mauti yalipomfika.

“Mhandisi Patrick Mfugale, alifariki tarehe 29 Juni 2021, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa baada ya kufariki ghafla. Kifo hiki cha ghafla kimetusikitisha sana,” amesema

Naye Vedasto Mfugale, mdogo wake na Mhandisi Patrick amesema, kifo hicho cha kaka yao kimewashtua na kuwasikitisha.

Amesema, mara baada ya kupata taarifa hizo, walikwenda hospitali ya Benjamin Mkapa na “tulipofika hospitalini, tuliambiwa amefika amekufa.”

Vedasto amesema, kila mmoja atafariki bila kujali atafariki dunia kwa njia ipi.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika msiba wa Mhandisi Patrick Mfugale

Kwa upande wa watoto wa marehemu, wamesema “huyu mzee wetu, aliipenda sana familia yake hapa Dar es Salaam na kule kijijini Ifunda. Ninyi mnamfahamu kama mtaalamu wa madaraja na barabara, sisi tulimfahamu kama baba mwema aliyeipenda familia.”

Wamesema, wamempoteza baba bora, mzalendo wa kweli kwenye taifa.

Mwili wa Mhandisi Mfugale, utazikwa nyumbani kwao Ifunga, Jumatatu ya tarehe 5 Julai 2021.

error: Content is protected !!