December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali: Laini za simu hazitafungwa

Spread the love

SERIKALI imesema, hakuna Mtanzania amabaye laini yake ya simu itafungwa kwasababu ya kutosajiliwa kwa alama za vidole. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Kauli hiyo ameitoa Kangi Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani, alipozungumza bungeni jijini Dodoma leo tarehe 13 Septemba 2019.

Amesema, ni maelekezo ya Rais John Magufuli kwamba, hakuna Mtanzania atakayezuiwa kutumia laini yake ya simu, kutokana na kukosa kitambulisho cha taifa, kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

“Kuhusu suala la kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole, na kwamba lazima uwe na kitambulisho cha taifa yaani NIDA, zoezi hilo lina muda wa mwisho wa Desemba mwaka huu.

“Lakini naomba tena niwatoe wasiwasi Watanzania wote kwamba, maelekezo ya mheshimiwa rais ni kuwa, hakuna Mtanzania ambaye simu yake itazuiwa kutumika ati kwasababu hana kitambulisho cha taifa na hivyo hajasajili laini yake,” ameeleza Lugola.

Lugola amesema, lengo la serikali ni kusajili kwa alama za vidole laini za Watanzania 24,500,000, na kuwa hadi sasa zaidi ya laini 20 milioni zimesajiliwa.

“Mheshimiwa mwenyekiti, lengo la usajili na utambuzi ilikuwa ni 24.5 milioni, lakini hadi sasa tumekwisha sajili Watanzania zaidi ya 20 milioni,” amesema Lugola.

Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilitangaza kuzifungia laini zisizosajiliwa kwa alama za vidole, ifikapo tarehe 31 Desemba 2019.

Sharti kubwa la kufanya usajili huo, ni kuwa na kitambulisho cha taifa au namba ya kitambulisho hicho, kinachotolewa na NIDA, ambapo baadhi ya Watanzania hawana, na hivyo kukwama kujisajili.

Wimbi la Watanzania wanaojitokeza kufuata taratibu za kupata kitambulisho hicho, limeongezeka katika maeneo mbalimbali yenye watumishi wa NIDA wanaotoa huduma hiyo. Huku baadhi yao wakikwama kutokana na kukosa cheti cha kuzaliwa.

Changamoto ya kukosa cheti cha kuzaliwa hasa kwa Watanzania waliozaliwa kuanzia miaka 1980 kwenda juu, imewakwamisha kupata huduma ya kusajiliwa katika baadhi ya vituo vya NIDA, kwa ajili ya kupata kitambulisho cha taifa.

error: Content is protected !!