May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kuwatoa kifungoni wafanyabiashara fedha za kigeni

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imesema itarejesha leseni za wafanyabiashara wa maduka ya kubadili fedha za kigeni, ili waendelee na shughuli zao. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 9 Julai 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Azam TV, jijini Dar es Salaam.

Kati ya 2019 na 2020, Serikali ilifanya msako kwa wafanyabiashara wa maduka hayo, katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na maeneo mengine, ili kubaini yaliyokuwa yanaendeshwa kinyume cha sheria na kusababisha makosa ya utakatishaji fedha.

Kupitia msako huo, baadhi ya wafanyabiashara walinyang’anywa leseni za uendeshaji maduka hayo, huku baadhi yao fedha zao zikichukuliwa.

Dk. Mwigulu amesema, amewaelekeza maafisa wa wizara hiyo kufanya tathimini juu ya suala hilo.

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba

“Nimeelekeza watu wetu wa kufanya evaluation (tathmini), warudishe leseni sababu kama wale watu wana uzoefu wa kuendesha ile shughuli, hatupaswi kuwakimbia tunapaswa tuwarudishe kazini. Tukiwarudisha kazini tutapa kodi,” amesema Dk. Mwigulu.

Waziri huyo wa fedha amesema, amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabishara hao.

“Nimewasilikiliza, nimeshakutana na baadhi yao tumeongea. Nimepokea hoja zao, moja ya hoja ambayo nimeipokea ni ile ambayo wanasema turudishe leseni na mimi nimelifanyia kazi,” amesema Dk. Mwigulu.

Aidha, Dk. Mwigulu amesema Serikali inalifanyia kazi ombi la wafanyabiashara hao, la kupunguziwa gharama za mtaji.

“Hoja ya pili wanasema kiingilio ama mtaji uliowekwa umekuwa juu sana, nimewaambia timu yangu ya watalaamu wafanye evaluation,” amesema Dk. Mwigulu.

error: Content is protected !!