May 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kuwapiga ‘tafu’ wanawake

Spread the love

SERIKALI imeahidi kuwaunga mkono wanawake wanaobuni miradi inayosaidia kutunza mazingira, ili waondokane na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi, anaandika Regina Mkonde.

Wakati akizindua mradi wa Green Voice Tanzania unaofadhiliwa na Taasisi ya Wanawake Afrika, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais amesema kuwa changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi zimekuwa zikiathiri maendeleo ya wanawake.

“Ninatambua jitihada za mradi na kwamba mimi kama meneja wa mazingira nchini nitahakikisha kwamba, serikali inaungana nanyi katika mapambano ya mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Samia na kuongeza;

“Natambua kwamba, kina mama na watoto wa kike wanapoteza muda mwingi kwenda kutafuta maji, kuni na mahitaji mengine na hii yote ni matokeo ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Kama muda huo wanaopoteza wangeutumia kufanya shughuli za kiuchumi na elimu zingesaidia kuwaletea maendeleo.”

Mama Samia amewataka wanawake kuzalisha kwa wingi bidhaa za kitanzania huku akiwataka watanzania kuwa wazalendo kwa kununua bidhaa zinazozalishwa nchini kwa lengo la kuwainua wajasiliamali wadogo.

“Kuna maofisa wetu wanaofanya kazi na taassisi za wanawake Tanzania, hao ndio waanzilishi wa majukwa ya wanawake na sisi kama serikali tunayatunza, wanawake wajiunge, wazalishe biashara za kitanzania, na wananchi wanunue bidhaa za kitanzania ili kuwawezesha,” amesema.

Getrude Mongella, Balozi wa Taasisi ya Wanawake Afrika amesema kuwa wakati nchi inapoelekea kwenye mapinduzi ya viwanda, wanawake wasibweteke na kushuhudia mapinduzi hayo yanafanywa na wanaume pekee.

“Lazima mapinduzi ya kiuchumi kupitia viwanda nchi yafanywe na jitihada za wanawake na si kwa wasomi tu, bali hata wanawake walio vijijini,” amesema.

Amewataka wanawake wenye uwezo kufanya jitahada za ujenzi wa viwanda vidogovidogo ambavyo vitakuwa vinasindika mazao yanayolimwa na wanawake wa vijijini ili kuwakomboa.

“Inabidi tujifunze kuzifanya changamoto kuwa fursa za kiamendeleo, mabadiliko ya tabia ya nchi ni changamoto inayosumbua mataifa mengi duniani na ndiyo maana mradi huu unalenga kuhakikisha kwamba dunia hususan Tanzania inarudi katika mazingira yake mazuri ya awali,” amesema.

Naye Malecela Balisidya, Mratibu wa mradi wa Green Voice Tanzania amesema kuwa licha ya mradi huop kuwa katika ngazi ya majaribio, umewasiadia wakina mama wengi ambao hivi sasa wanajihusisha na ujasiliamali.

“Mradi huu unafadhiliwa na aliyekuwa makamu wa rais wa spain yeye ana taasisi iliyotenga fedha ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi afrika, akianzia na Tanzania, na kwamba mradi huu umefadhili wanawake kumi na watano ambao wamefundishwa jinsi ya kutunza mazingira yetu na rasilimali,” amesema.

Wamejiingiza kwenye ufugaji nyuki, upandaji bustani, leo hii tulikuwa tunazindua baada ya kuona walichokifanya, walikuwa kumi na tano na wamefundisha wenzao 250.

 

error: Content is protected !!