December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kusajili upya maduka ya fedha za kigeni

Spread the love

SERIKALI imesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itaanza kusajili upya maduka ya kubadili fedha za kigeni. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza mkoani Arusha jana tarehe 17 Mei 2019, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema BoT inakamilisha zoezi la kuratibu utoaji vibali vya uendeshaji , na kwamba zoezi hilo likikamilika, maduka yaliyofungwa yataruhusiwa kuendelea na biashara hiyo.

Waziri Majaliwa amesema awali serikali ilifunga maduka hayo ili kuratibu vizuri mfumo wa udhibiti wa matumizi ya dola nchini, ikiwemo kuondoa biashara holela za ubadilishaji fedha za kigeni.

“Baada ya serikali kuratibu vizuri mfumo wa udhibiti wa matumizi ya dola hapa nchini, unaolenga kuondoa mzagao wa biashara ya dola kiholela. Kwa sasa tumeendelea kuratibu.  Tumeanza na mabenki, baada ya uhakiki unaoendelea tutatoa fursa kwa mfanyabiashara mmoja mmoja,”amesema Waziri Majaliwa.

Waziri Majaliwa amesema pindi uratibu huo utakapokamilika, serikali itatoa leseni za ufanyaji biashara ya kubadili fedha za kigeni katika maeneo ya kimkakati.

“Niseme tu hata kwa wale ambao walikuwa wanafanya biashara hiyo na shughuli zao zimesimama,  benki kuu inakamilisha uratibu wao na mawasiliano yao. Ili baadae iweze kuratibu vizuri na kutoa utaratibu mzuri wa kutoa vibali vya uendeshaji wa maduka hayo,” amesema Waziri Majaliwa na kuongeza.

 “Wasiwe na mashaka utaratibu unaendelea, kwenye maeneo ya kimkakati ili tuwe na maduka tunayoyafahamu yaliyo sajiliwa vizuri na yanaweza kufanya biashara hiyo vizuri kuliko ilivyokuwa awali.”

Mwishoni mwa mwaka 2018 BoT ilifunga maduka zaidi ya 100 hasa mkoani Arusha, baada ya wamiliki wa maduka hayo kubainika kwamba hawajakidhi masharti ikiwemo kutokuwa na leseni halali za kufanya biashara hiyo.

error: Content is protected !!