SERIKALI ya Tanzania, kesho tarehe 3 Oktoba 2023, inatarajia kupokea ndege mpya ya masafa ya kati aina ya Boeng 737-9, ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), pamoja na ndege mbili ndogo za mafunzo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 2 Oktoba 2023, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ambapo hafla ya mapokezi hayo itafanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini humo.
Prof. Mbarawa amesema ndege hizo ni miongoni mwa ndege nne mpya ambazo Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, iliingia mkataba na Kampuni ya Boeng ya Marekani, kwa ajili ya utengenezaji Julai 2021.
Ndege hizo ni mbili za abiria za masafa ya kati aina ya Boeng 737-9 yenye uwezo wa kubeba abiria 181 kila moja, ndege moja ya abiria ya masafa marefu ya Boeng 787-8 Dreamliner (abiria 262) na ndegemoja kubwa ya mizigo ya Boeng 767-300 yenye uwezo wa kubeba tani 54.

“Serikali yetu chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia, imeendelea kuhakikisha kuwa ATCL inatoa huduma zenye kuhimili ushindani kwa kuanzisha safari za moja kwa moja kwenda kwenye masoko ya kikanda na kimataifa,” amesema Prof. Mbarawa.
Waziri huyo wa uchukuzi amesema kuwasili kwa ndege hiyo ya abiria kutafanya idadi ya ndege za ATCL kuongezeka kutoka 13 hadi 14. Amesema ndege nyingine mbili zilizosalia zinaendelea kutengenezwa nchini Marekani, zinatarajiwa kuwasili nchini Desemba 2023 na Machi 2024.
Amesema ujio wa ndege hiyo, kutaifanya ATCL kuhudumia vituo vya ndani 14, vituo vya kikanda na kimataifa vikiwemo vya Nairobi (Kenya), Bunjumbura (Burundi), Ndola na Lusaka (Zambia), Lubumbashi (DRC).
“Utasaidia kuongeza miruko ya safari za usiku kwa viwanja vya ndege vyenye taa, kuanzisha safari za usiku katika viwanja vya ndege vya Dodoma na Songea, ambapo miradi ya ufungaji taa inakamilika. Aidha, ATCL itaendelea na miruko yake ya kimataifa na itaanzisha safari mpya za Goma, Lagos Nigeria,” amesema Prof. Mbarawa.
Leave a comment