January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kukagua vibali vya ajira kwa wageni

Spread the love

MUDA wowote kuanzia sasa serikali imepanga kuanza ukaguzi wa vibali vya ajira za wageni nchini. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Uamuzi huo unatokana na kuisha kwa muda wa siku 14 uliotolewa na serikali katika tangazo la utolewaji wa vibali vya kazi kwa wageni nchini lililotiwa saini tarehe Desemba 14, mwaka huu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Aiira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama (Mb).

Katika tangazo hilo, Mhagama aliwataka waajiri wote nchini ndani ya siku hizo wawe wametekeleza matakwa ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015.

“Katika taarifa tuliyoitoa mwezi huu, tuliwajulisha waajiri wote wenye waajiriwa wageni ambao wana vibali vya kazi za muda (Carry on Temporary Assignment) na wale wote wasiokuwa na vibali vya ajira vilivyotolewa na kamishna wa kazi nchini kuwa, wanatenda kosa.

“Kamishna wa kazi amepewa mamlaka kutoa vibali vya ajira kwa wageni wanaotaka kufanya kazi nchini na kwamba, hakuna mamlaka nyingine inayoruhusiwa kutoa vibali vya ajira kwa wageni,” amesema Mhagama

Mhagama amesema hayo wakati akizungumza na kikosi maalum kitakachoendesha operasheni hiyo chenye wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA).

Lengo ni kufuatilia kama agizo lililotolewa na serikali limefuatwa na kuhakikisha taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa vibali vya ajira zinazingatiwa.

“Serikali ilitoa muda wa siku 14 kwa waajiri wote wawe wametekeleza matakwa ya Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” amesisitiza Mhagama.

Mwezi Machi mwaka huu Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015 (The Non-Citizens (Employment Regulation) Act)).

Sheria imeanza kutumika rasmi tangu tarehe 15 Septemba, 2015. Sheria hiyo inaanzisha mamlaka moja ya utoajiwa vibali vya ajira kwa wageni na mamlaka hiyo ni Kamishna wa Ajira.

error: Content is protected !!