May 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kujenga mabwawa 88

Spread the love

 

BWAWA la Choma cha Nkola lipo katika Kijiji cha Choma, Kata ya Choma iliyopo Wilaya ya Igunga, Tabora lina uwezo wa kutunza maji mita za ujazo 6,825,757 na maji haya yanaweza kumwagilia hekta 400 za mpunga. Anaripoti Jemima Samwel DMC … (endelea).

Bwawa hilo ni miongoni mwa mabwawa 88 yaliyopo kwenye andiko la programu ya ujenzi wa mabwawa katika mikoa kame Tanzania Bara, yanayotarajiwa kujengwa.

Ni kauli ya Adolf Mkenda, Waziri wa Kilimo wakati akijibu swali la Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga ambaye ameihoji serikali lini itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa makubwa na skimu ya umwagiliaji Choma, Chankola leo tarehe 29 Aprili 2021.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkenda amesema, tayari usanifu umefanyika na kuonesha kwamba bwawa hilo lina uwezo wa kulisha eneo kubwa la mashamba ya mpunga.

Awali, mbunge huyo alisema serikali inatakiwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo.

“Je? Ni lini serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa makubwa na skimu ya umwagiliaji Choma Chankola, Ziba na Simbo ambayo yamefanyika upembuzi yakinifu kwa zaidi ya miaka sita sasa?” amehoji.

Prof Adolf Mkenda, Waziri wa Kilimo

Waziri Mkenda amesema, bwawa la Choma cha Nkola pamoja na mabonde yote ya Ziba yanayofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, yameingizwa kwenye Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa mwaka 2018 kwa ajili ya utekelezaji wake na kwamba, serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo.

” Bwawa la Simbo lililopo Kijiji cha Simbo, Kata ya Simbo wilayani Igunga; usanifu wake umekamilika. Bwawa hili lina uwezo wa kutunza maji mita za ujazo 15,228,318 na maji yaliyovunwa yanaweza kumwagilia hekta 1,000 za mpunga. Bwawa hili pia lipo kwenye Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Mwaka 2018 kwa ajili ya utekelezaji wake,” ameeleza Mkenda.

error: Content is protected !!