SERIKALI ya Tanzania, inatarajia kutangaza masharti mapya ya usajili wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, ili kuchochea ukuaji wa biashara hiyo nchini. Anariupoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 24 Juni 2022, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande, akimjibu Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba, aliyehoji mkakati wa Serikali katika kupanua biashara ya ubadilishaji fedha za kigeni ili kuboresha huduma hiyo kwa raia wa kigeni hasa watalii.
Chande amesema, kwa sasa watalaamu wa Wizara ya Fedha na Mipango, wako katika hatua za mwisho za kuchakata masharti hayo na kwamba hivi karibuni yatatangazwa, huku akiahidi kwamba yatakuwa nafuu.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyofanya kutangaza utalii na vivutio vyetu ndani ya nchi yetu. Serikali tumezingatia suala lako la kupunguza masharti, wataalamu wamekaa na wanachakata. Hivi karibuni yatatoka masharti nafuu sana kwa ajili ya wawekezaji wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni,” amesema Chande.
Katika hatua nyingine, Chande amejibu swali la Tarimba lililohoji lini Serikali itaondoa changamoto ya tofauti ya gharama za kubadilisha fedha za kigeni hasa Dola za Marekani, akisema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (B.o.T), itatoa bei elekezi.
Leave a comment