October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kuboresha sera ya mbegu

Mahindi yakiwa shambani

Spread the love

SERIKALI imesema ina mpango wa kuboresha sera ya mbegu ili kuimarisha suala la upatikanaji wa mbegu kimfumo zitakazowasadia wakulima na kuleta tija katika kilimo nchini. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Hayo yalisemwa na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Raphael Chibunda kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwe wakati akifunga mdahalo wa mbegu uliowahusisha wataalamu wa mbegu, wazalishaji, wasimamizi, wauzaji na wakulima ulioandaliwa na Wizara ya Fedha Tanzania kupitia mradi wa mabadiliko ya tabia nchi uliofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya.

Alisema, katika kutekeleza maelekeo ya Serikali ya Awamu ya Tano lengo kubwa ni kuimarisha kilimo ili kichangie katika ujenzi wa viwanda na kwamba kujadili suala la mfumo wa mbegu kutaleta manufaa.

Prof. Chibunda alisema kwa sasa Serikali inafanya mapitio ya sera za kilimo ambapo wao wameibua mjadala wa masuala ya kuboresha sera ya mbegu na Wizara itayachukua na kuboresha sera ambazo zitatekelezwa ili kuimarisa upatikanaji wa mbegu bora ambazo wakulima watakuwa na uwezo wa kuzinunua ili kuboresha kilimo nchini.

Naye Mratibu wa mradi huo alisema, Grace Aloyce kufuatia umuhimu wa suala la mbegu nchini ni muhimu kuwaita wadau wote sekta ya kilimo wakiwemo sekta binafsi, serikali na taasisi za kiraia ili waweze kuchangia kwenye sera ya kilimo ambayo ipo kwenye maandalizi kwa sasa.

Alisema, kupitia mradi wa mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika jijini Dodoma waliweza kubaini kuwa awali wakulima walipata changamoto ya mbegu ambapo walitumia mbegu mbalimbali na kukosa mazao inavyotakiwa kufuatia kupanda mbegu ambazo inapokosekana mvua hukosa mavuno kabisa.

Alisema, baada ya baadhi ya wakulima kununua mbegu bora zilizoboreshwa waliweza kuvuna na kupata na kipato cha kusomesha watoto wao na manufaa mengine na wengine walikosa kununua mbegu hizo.

“Sasa tumeona kwamba wengi wamekosa mbegu hizo zilizoboreshwa, huenda ni kutokana na aidha kwa kukosa uwezo au kwa ukosefu kujua kuwa wapi wanaweza kupata mbegu hizo,” alisema.

Alisema, kupitia mkutano huo wakulima wanaweza kunufaika kwa kupata mbegu kwa bei nzuri na kuweza kujua zinapopatikana ili kukabiliana na changamoto ya kukosa mazao bora kutokana na kukosa mbegu jambo ambalo wakati mwingine husababishwa na ukosefu wa  kipato.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi Udhibiti wa ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI) Patrick Ngwediagi kwa niaba ya wataalamu wa mbegu walioshiriki mdahalo huo na kutoa mapendekezo yao, aliiomba Serikali na wadau wa mbalimbali kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi hasa kwenye upatikanaji wa mbegu zinazokabiliana na hali hiyo.

Pia alisema, wameazimia kuwe na juhudi kubwa za kuboresha upatikanaji wa mbegu ikiwa bora kwa kupitia sheria zilizopo ambapo inapaswa udhibiti wa ubora wa mbegu uimarishwe ili wakulima wanufaike na wanachokipanda.

Hivyo aliiomba Serikali kuboresha sera na sheria zilizopo ili kuhakikisha mbegu zinapatikana kwa wingi na kuwafikia wakulima huku wakulima wakiondokana na matatizo ya upatikanaji wa mbegu hafifu na feki.

error: Content is protected !!